Na; Daudi Manongi -MAELEZO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Kapt. Mstaafu George Mkuchika amesema kuwa maendeleo yaliyopatikana nchini  yametokana na  Utawala bora unaosimamiwa vyema na Serikali ya awamu ya tano.

Akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari-MAELEZO Waziri Mkuchika amesema kuwa Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi ya maendeleo kutokana na kuwepo kwa utawala bora.

“Katika miaka mitatu  ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe.John Pombe Magufuli  ameonyesha  mfano bora katika kusimamia utawala bora ambapo Tanzania imeshika nafasi ya 17 kati ya nchi 54 za Afrika katika kusimamia  na kutekeleza dhana ya utawala Bora kwa mujibu wa ripoti ya Mo Ibrahim”alisema Mkuchika.

Amesema tathmini ya utawala bora katika miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano imeleta sura nzuri nchini ambayo imechangiwa na utashi wa kisiasa ambapo katika awamu zote tano zimesimamia suala hilo.

 Mhe. Mkuchika amesema kuwa nidhamu ya watumishi wa umma imeimarika nchini hali inayoongeza tija katika huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Aliongeza kuwa  Taasisi za nje na ndani ya nchi zimeonesha kuwa suala la rushwa nchini limepungua  kufuatia hatua za makusudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha utawala Bora.

“Shilingi bilioni 127 zimeokolewa na serikali  kwa kuzuia vitendo vya rushwa ambapo mali zenye thamani ya shilingi bilioni 4.5 zimezuiliwa na Serikali” aliongeza Mkuchika.

Aidha, ameongeza kuwa Taasisi za kimataifa zimeonesha kuwa Tanzania inafanya vizuri katika kusimamia na kutekeleza  dhana ya utawala bora. Utawala Bora umeisaidia nchi yetu kuongeza makusanyo ya kodi,kununua ndege ,kuondoa watumishi hewa,kuanzishwa kwa mahakama ya mafisadi na kufutwa  kwa matumizi yasiyo ya lazima.

Kipindi cha TUNATEKELEZA kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO ambapo awamu hii inawahusisha Waheshimiwa Mawaziri.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: