Rais Donald Trump wa Marekani amekutana na mwezake wa Kenya Uhuru Kenyatta mjini Washington na kuzungumzia masuala mbalimbali, zaidi wakiangazia biashara na usalama.

Kwa mujibu wa taarifa ya ikulu ya Marekani, wakati wa ziara hiyo mataifa hayo mawili yalikubaliana na kutangaza mikataba ya jumla ya $900 milioni.

Hata hivyo mazungumzo yao yaligubikwa na msiba wa aliyekuwa mgombea wa Urais wa Marekani na Seneta wa muda mrefu katika bunge la nchi hiyo John McCain.

Rais Kenyatta ni kiongozi wa tatu kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara kukaribisha Ikulu ya White House na kufanya mazungumzo na Rais Trump.

"Tumekuwa na ushirikiano mzuri na wa kipekee na Marekani katika masuala ya usalama na ulinzi, hasa katika harakati za kukabiliana na ugaidi. Muhimu zaidi tuko hapa kuboresha ufungamano wetu katika biashara na uekezaji, " kasema Rais Kenyatta.



Rais Trump alisema Kenya na Marekani zitaendelea kushirikiana kuimarisha ufungamano wao katika biashara, uekezaji na usalama.

"Tunafanya shughuli nyingi za utalii, biashara na ulinzi. Na kwa wakati huu tunajibidiisha kuboresha usalama," alisema Rais Trump. " Tunafurahia sana kuwa nawe hapa."

Viongozi hao wawili walijadiliana pia kuhusu safari za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi New York zitakazoanza mwezi Oktoba mwaka huu na kukubaliana kwamba safari hizo za ndege zitaimarisha zaidi utalii na biashara kwa manufaa ya nchi hizi mbili.

Marekani ndiyo chanzo kikuu cha watalii wanaozuru Kenya na taifa hilo la Afrika Mashariki linatarajia kutumia fursa ya safari za moja kwa moja za ndege za Kenya Airways kati ya mataifa hayo mawili ambazo zitaanza Oktoba 28 kuimarisha idadi ya watalii wanaofika kenya.

Viongozi hao wawili kwa pamoja wamejadili njia za pamoja za kupambana na ugaidi na ushirikiano wa kibiashara.

Mpango wa upanuzi wa barabara inayohusisha miji mikubwa ya Kenya, Mombasa na Nairobi pia ilijadiliwa.

Kwa upande wake Rais Uhuru Kenyatta ameandika katika mtandao wa Twitter kwamba amefanikisha makubaliano yenye thamani ya mamilioni ya dola na Wawekezaji wa Kimarekani.

Katika siku za hivi karibuni China imeipita Marekani kwa kuwa na uwekezaji mkubwa nchini Kenya.

Hata hivyo Rais Kenyatta ameonekana kuwa na bidii ya kuwakubali washirika wote kibiashara.

Kibiashara, Kenya ni ya 85 kwa kuiuzia Marekani bidhaa duniani na wa jumla biashara kati ya mataifa hayo mawili huwa ya thamani ya jumla ya dola 1.5 bilioni za Marekani kwa mujibu wa Wizara ya Biashara ya Marekani.

Kenya imekuwa ikitafuta ufadhili wa ujenzi wa barabara mpya kuu ya kutoka Mombasa hadi Nairobi, mradi unaotarajiwa kugharimu takriban dola 4.5 bilioni za Marekani.

Kenya hutazamwa kama mshirika muhimu wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi Afrika Mashariki na katika Upembe wa Afrika.

Mataifa yote mawili yana majeshi Somalia yakikabiliana na wapiganaji wa al-Shabaab.

Baadaye wiki hii pia anatarajia kumpokea jijini Nairobi, Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, kabla ya kufunga safari kuelekea Beijing, kwenye mkutano wa pamoja wa Afrika na China.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: