Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemkuta na kesi ya kujibu aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Tido Mhando.

Katika kesi hiyo inayomkabili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya shilingi milioni 887.1 ambapo ataanza kujitetea September 20.

Uamuzi huo umetolewa leo Agosti 27 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashtaka na hivyo Tido ataanza kujitetea Septemba 20, 2018.
Miongoni mwa  mashahidi  wa upande wa mashtaka ambao wametoa ushahidi katika kesi hiyo ni ofisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa, mkurugenzi mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana na Dominic Maundi. 
Katika kesi hiyo inadaiwa Juni 16, 2008, akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.
Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.
Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.
Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Katika shtaka la mwisho, anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh887,122,219.19. Tido yupo nje kwa dhamana.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: