Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini asubuhi hii kuelekea Harare nchini Zimbabwe ambapo anakwenda Kumuwakilisha  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwenye  Sherehe za kuapishwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe.Emmerson Mnangagwa zinazofanyika leo tarehe 26 Agosti, 2018 katika uwanja wa michezo waTaifa Mjini Harare.
 
Akizungumza kabla ya kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini DSM, Mhe.Rais Mstaafu  Kikwete ambaye amefuatana na  Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (Bara) Ndg. Philip Mangula na Mwenyekiti wa Chama cha UDP Ndg. John Cheyo , amesema Tanzania na Zimbabwe zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu  wa kindugu kwani katika kipindi ambacho Zimbabwe ilikuwa ikidai uhuru, baadhi ya wananchi wake  waliwahi kuishi nchini Tanzania, husasani wanachama wa Chama cha ZANU PF, na kupata mafunzo hapa nchini.
 
‘’Baadhi ya wanajeshi wetu wameshiriki pamoja na wanajeshi wa Zimbabwe katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe na ndio maana kwenye Jeshi letu kuna medani ya Zimbabwe’’ amesema Rais Mstaafu Kikwete.
 
Rais Mnangagwa anaapishwa leo kuongoza taifa la Zimbabwe baada ya kushinda katika uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika tarehe 30 Julai, 2018

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Agosti, 2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: