Rais  Dk. John Magufuli amemwelezea dada yake marehemu Monica Joseph kuwa alikuwa mtu mwenye upendo kwa familia yao na tegemeo kubwa la kumtunza mama yao mzazi, Suzana Ngolo Magufuli kwa kukubali kuondoka nyumbani kwa mumewe kwa zaidi ya miaka miwili.

Alisema marehemu Monica ameacha somo kwa watoto wote na wanandoa kwa kuwa tayari kujitolea kuwalea wazazi wao wanapokabiliana na changamoto za uzee badala ya kuwaacha wakitaabika.

Alisema hayo wakati akitoa shukrani kwa mamia ya waombolezaji waliohudhuria maziko hayo yaliofanyika kijijini kwao Mlimaji, wilayani Chato mkoani Geita.

“Mmetuonyesha upendo mkubwa sana na kweli ujio wenu na kuungana nasi katika tukio hili mmetufariji sana, asante sana kwa upendo huu na Mungu awabariki sana,” alisema.

Viongozi mbalimbali wa chama na serikali ndani na nje ya nchi, jana walihudhuria maziko hayo yaliyofanyika katika makaburi ya familia.

Katika maziko hayo, misa takatifu iliongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Mhashamu Severine Niwemugizi aliyeambatana na maaskofu wengine saba.

Viongozi waliohudhuria maziko hayo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Marais wastaafu wa awamu ya pili, tatu na nne, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete.

Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Philip Mangula, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, mawaziri, wabunge, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa madhehebu ya dini, vyama vya siasa, mikoa na wilaya.

Akisoma wasifu wa marehemu kwa niaba ya familia, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, alisema marehemu Monica alikuwa mtoto wa kwanza wa mzee Joseph Marco Magufuli na mama Suzana Ngolo Magufuli.

Alisema Monica ameacha mume, watoto tisa na wajukuu 25.

Share To:

Anonymous

Post A Comment: