Chama cha Mapinduzi (CCM), kimemtaka mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari kutofikiria kuomba kujiunga nacho kwa madai kuwa hana viwango vinavyoendana na CCM.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alitoa kauli hiyo jana asubuhi wakati akihojiwa na kituo kimoja cha redio.

Kauli hiyo ya Polepole ilitokana na watangazaji wa kipindi hichokutaka kujua ukweli wa tuhuma zilizowahi kutolewa na Nassari juu ya CCM kushiriki mchezo mchafu wa kuwanunua madiwani kutoka Chadema.

Watangazaji hao walitaka kufahamu upi msimamo wa CCM kuhusu tuhuma hizo na kauli aliyowahi kuitoa aliyekuwa mkuu wa Wilaya wa Arumeru, Alexander Mnyeti kuwa Nassari naye kama anataka ‘kununuliwa’ aende dau lake ni kubwa.

Mtangazaji aliuliza, “kama unachosema ni kweli kwamba CCM hainunui wapinzani ni ipi kauli yenu kuhusu madai ya Nassari na kauli aliyoitoa Mnyeti kuwa fedha zipo wanaotaka kununuliwa waende na dau la Nassari ni kubwa?”

Akijibu swali hilo, Polepole alisema, “kwanza huyo Nassari asifikirie kuja CCM maana hana viwango vyetu na kule Arumeru Mashariki asubiri 2020 kuna mtu wetu tumemuandaa anaenda kulichukua lile jimbo.”

Nassari alipotafutwa  kuzungumzia kauli hiyo alijibu kwa kifupi, “ukiwa safarini kama nilivyo mimi nikiwahudumia watu wa Meru halafu akatokea mbwa anabweka ukimrushia mawe utapoteza muda kufika safari yako, hivyo huyo nampuuza maana hajui anachokifanya.”

Kuhusu hamahama ya wabunge na madiwani wanaotoka upinzani kwenda CCM, alisema hilo ni suala la utawala bora na si kweli kwamba marudio ya uchaguzi yanaharibu bajeti nyingine.

“Pesa ya uongozi bora ipo, si kweli kwamba tunapofanya uchaguzi pesa ya elimu inapunguzwa, hapana. Ndiyo sababu Tume ya Uchaguzi ina bajeti yake ila tatizo linakuja hapa ikiwa upande wa CCM, ila wakifanya vyama vingine inaonekana ni sawa,” alisema.

“Juzi Chadema imewafukuza madiwani wake kule Mbeya, lakini hilo halionekani kuwa tatizo wala kuleta hasara maana lazima uchaguzi utafanyika ila ikifanya CCM inaonekana nongwa, hizi ni siasa za double standard.”

Polepole pia alizungumzia suala la wapinzani wanaohamia CCM kusimamishwa kwenye uchaguzi na kueleza kuwa msingi wa chama hicho unasisitiza usawa kwa wote, hivyo hata wanaohamia wana haki ya kuchagua au kuchaguliwa.

Alisema wagombea wote wanaosimamishwa kanuni na taratibu za chama hicho zinazingatiwa na anashangazwa na watu wanaoonekana kuguswa na mambo yanavyokwenda ndani ya CCM.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: