Mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ibutamisuzi, Kata ya Mbutu wilayani Igunga Mkoa wa Tabora, Nchambi Malunde (9), amenusurika kufa baada ya kujeruhiwa vibaya na fisi wakati akienda shuleni na mwanafunzi mwenzake.


Mama wa mwanafunzi huyo, Masaaka Mwandu, alisema tukio hilo lilitokea Ijumaa majira ya asubuhi wakati mwanaye akiwa na mwanafunzi mwenzake wa darasa la kwanza ambaye hata hivyo, hakumtaja jina wakiwa njiani kwenda shuleni ndipo walipovamiwa na fisi.


Alisema baada ya fisi huyo kuwavamia, alianza kumng'ata mwanae, hivyo kupiga kelele kuomba msaada, hali iliyomfanya mwanafunzi mwenzake kutimua mbio kwenda kutoa taarifa kwenye nyumba ya jirani ambapo wananchi walifika eneo hilo wakiwa na mikuki, mashoka, mapanga na marungu.

Kwa mujibu wa Mwandu, pamoja na wananchi kufika kwenye eneo la tukio na kuanza kumfukuza fisi huyo, aliamua kumuachia mwanafunzi na kuwageukia wananchi akiwatishia kuwashambulia kisha kutoweka na mfuko wa madaftari ya mwanafunzi huyo.

Mama huyo alisema baada ya fisi kutoweka, ndipo wananchi walipomchukua mwanae na kumpeleka nyumbani ili apelekwe Hospitali ya Wilaya ya Igunga kwa matibabu, lakini kabla hawajaondoka fisi huyo alifika nyumbani kwa mwanafunzi huyo huku akiwa na mfuko wa madaftari mdomoni na ndipo wananchi walimfukuza tena.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ibutamisuzi, Ludovick Ngassa, alisema baada ya kumuokoa mwanafunzi huyo waliamua kupiga simu Idara ya Maliasili kuomba msaada na ndipo maofisa wanyamapori walifika kijijini hapo na kuanza kumsaka fisi huyo bila mafanikio.


Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi, Ibutamisuzi, Alex Simumba, alithibitisha kwamba mwanafunzi huyo anasoma katika shule hiyo na kuiomba Idara ya Maliasili kumsaka fisi huyo hadi apatikane ili kunusuru maisha ya wanafunzi wengine.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Merchades Magongo, alithibitisha kumpokea Nchambi akiwa amejeruhiwa vibaya sehemu za begani, maeneo ya makalio na kusema kuwa amelazwa wodi namba nane na hali yake si nzuri na kwamba majeraha aliyonayo ni makubwa.


Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Wilaya ya Igunga, Jahulula Edward, alisema baada ya kupewa taarifa na mtendaji wa kijiji hicho juu ya fisi huyo, walikwenda hadi eneo hilo ambapo kwa kushirikiana na wananchi walimtafuta bila mafanikio na kuongeza kuwa wanaendelea kumsaka hadi apatikane.


Kwa mujibu wa Jahulula, pamoja na kumjeruhi mwanafunzi pia fisi huyo alimshambulia ndama hadi kufa, na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi watakapomuona fisi huyo.
Share To:

Anonymous

Post A Comment: