Mkuu mpya wa wilaya Nyamagana Mhe. Dkt. Philis Misheck Nyimbi (kulia) akila kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. John Mongella (kushoto). Mhe. Dkt. Nyingi amechukua nafasi ya Mhe.Marry Tesha.

Judith Ferdinand Mwanza. 

Wakuu wa wilaya zote mkoani Mwanza wametakiwa kutimiza vyema majukumu yao na kuhakikisha kuna ukusanyaji na usimamiaji madhubuti wa mapato.
Mkuu wa mkoa Mwanza Mhe.John Mongella ametoa agizo hilo leo wakati akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya za Nyamagana, Ilemela, Magu na Ukerewe walioteuliwa hivi karibuni na Rais Dkt.John Pombe Magufuli.

Mhe.Mongella alibainisha kwamba katika majiji sita nchini, Jiji la Mwanza ni la tani kwa ukusanyaji wa mapato huku Manispaa ya 
Ilemela ikishika nafasi ya tatu kutoka mwisho miongoni mwa Manispaa zote.
Aidha Mhe.Mongella aliwasisitiza wakuu hao wa wilaya kufanya kazi kwa uadilifu huku wakifuata  misingi ya kazi kwa kuhakikisha ulinzi, usalama, utulivu na kuhamasisha maendeleo katika wilaya zao.

Mkuu wa wilaya Ilemela, Mhe. Dkt. Severine Lalika alimshukuru Rais Dkt.Magufuli kwa kumteua katika nafasi hiyo na kuahidi ushirikiazo na viongozi mbalimbali katika kutatua kero na kuleta maendeleo kwa wananchi wa wilaya hiyo.

“Mtu mmoja hawezi kuleta maendeleo, hivyo nitashirikiana na Manispaa ya Ilemela akiwemo Mkurugenzi na baraza la madiwani kwenye vipaumbele vyao kwani naamini ndipo changamoto na kero za wananchi zilipo, pamoja na  kamati ya ulinzi na usalama ili kuhakikisha wilaya inakuwa salama”. Alisema Mhe.Dkt. Lalika.

Naye mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mhe. Dkt. Philis Nyimbi alisema ili waweze kufanya kazi vizuri ataendeleza mikakati mizuri iliyopo na kuongeza mikakati mipya huku akisimamia vyema ajenda ya viwanda kwa kuendeleza vilivyopo na kuanzisha vipya pamoja na kutumia taaluma yake kuwasaidia wananchi wa wilaya hiyo katika sekta ya afya.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya Magu Mhe. Philemon Sengati aliahidi kufanya kazi kwa bidii huku akishirikiana na viongozi mbalimbali katika kutatua kero za wananchi wa wilaya hiyo hususani maji, kilimo na ufugaji.

Aidha mkuu wa wilaya Ukerewe, Mhe. Cornel Magembe alisema ataitumikia nafasi hiyo kwa kasi anayohitaka Rais Magufuli na kuahidi kupambana na suala la uvuvi haramu katika visiwa vyote 32 vya wilaya hiyo.
Share To:

Post A Comment: