Tuesday, 14 August 2018

Mbowe Na Vigogo Wengine CHADEMA Waiomba Mahakama ya Kisutu Isitishe Kusikila Kesi Yao

Viongozi 9 wa Chadema akiwemo mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wamewasilisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu maombi ya kuomba kesi yao ya jinai namba 112/2018 kuahirishwa hadi rufaa yao itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Pia, wameomba kesi hiyo iahirishwe hadi maombi yao ya kutaka kesi iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu isitishwe usikilizwaji wake hadi hapo rufaa yao itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani.

Maombi hayo yamewasilishwa mahakamani hapo leo Jumatatu Agosti 13, 2018 mbele ya mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri na mawakili wa upande wa utetezi. Jeremiah Mtobesya na Peter Kibatala.

Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango ameieleza mahakama kuwa wamepewa hati ya maombi hayo namba10/2018 na kwamba wapo tayari kuwasilisha majibu kinzani kesho na kuwapatia upande wa utetezi.

Wakili wa utetezi Mtobesya naye aliomba wapewe siku mbili ili waweze kufaili majibu ya nyongeza kama watakuwa nayo.

Baada ya kusikiliza pande zote, Hakimu Mashauri aliamuru upande wa mashtaka kuwasilisha majibu kinzani Agosti 14, 2018  na iwapo upande wa utetezi  utakuwa na majibu ya nyongeza wayawasilishe Agosti 16,  2018.

Hakimu Mashauri amesema maombi hayo yatasikilizwa Agosti 21, 2018 na kwa upande wa kesi ya msingi nayo pia itatajwa mahakamani hapo Agosti 21, 2018.

Wakati hayo yakiendelea washtakiwa wote walikuwepo mahakamani.

Washtakiwa hao wamekata rufaa Mahakama ya Rufani wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kutupilia mbali maombi yao ya marejeo dhidi ya maamuzi madogo yaliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment