Monday, 27 August 2018

Halmashauri ya Ilemela yajipanga kudhibiti udanganyifu Mtihani wa Taifa Darasa la saba


Na James Timber, Mwanza
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, imejihakikishia  kuepuka na udanganyifu katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba  unaotarajia kuanza Septemba 3 hadi 6 mwaka huu.

Akizungumza wakati katika Kikao cha Robo ya Nne ya Mwaka wa Fedha 2017/2018 cha  Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Ilemela Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo John Wanga, aliwahakikishia madiwani kuwa hakutakuwa na udanganyifu utakaofanywa katika mtihani huo.

 "Naomba viongozi wa ngazi zote kutoa ushirikiano wakati wa zoezi hili ili wanafunzi waweze kufanya mtihani kwa amani na bila udanganyifu wa aina yoyote kwani tangu mwaka 2016 hakuna taarifa za kuvuja kwa mitihani katika halmashauri hii naomba watahiniwa wafuate sheria zilizowekwa na Baraza la Mitihani," alisema Wanga.

Wanga alisema jumla ya watahiniwa  8904 wavulana 4195 na wasichana 4709 kutoka shule za msingi 107 kutoka halmashauri hiyo wanatarajia kufanya mthihani huo ambapo watahiniwa 7518 wavulana 3486 na wasichana 4032 kutoka shule za msingi za serikali 74 huku jumla ya  watahiniwa 1386 kutoka shule binafsi 33 wavulana wakiwa 709 na wasichana 677.

Naye Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Diwani wa Kata ya Ilemela Willbard Kilenzi alisema, kuwa kuna malalamiko na minongono  kuwa kuna baadhi ya shule za binafsi na serikali zimekuwa zikifanya udanganyifu katika mitihani ya taifa ili waonekane wanafanya vizuri.

Aidha Kilenzi alisema, kufatia malalamiko hayo halmashauri iweze kufanya uchunguzi na wakibaini kuwa siyo kweli waweke mazingira ya kutoweza kutokea ila ikithibitika ni kweli hatua ziweze kuchukuliwa na kudhibiti.

Hata hivyo halmashauri hiyo imeshika nafasi ya pili kimkoa katika mtihani wa majaribio moko  wa darasa la saba mwaka huu.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: