Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ameagiza makontena 20 ya samani yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda, yapigwe mnada ikiwa ni sehemu ya kusimamia sheria na kanuni za kodi zilizopo nchini.

Mh. Mpango ametoa maelekezo hayo leo alasiri kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA alipofanya ziara ya kushtukiza na kukagua makontena hayo katika Bandari Kavu ya Dar es Salaam (DICD).

Aidha, Waziri Mpango ameweka wazi kwamba hajali vitisho vya mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam na ameapa kuendelea kusimamia sheria na kanuni za kodi nchini na hilo halichagui mtu wala nafasi yake.

Akiwa kwenye ibada jana huko Wilayani Ngara mkoani Kagera Mh. Paul Makonda alitoa onyo kwa mtu atakayenunua makontena hayo yenye samani za ndani kama vile meza, viti na mbao za kufundishia atapata laana lakini Waziri amesema hatojali vitisho hivyo.

Tangazo la TRA lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News Mei 12, liliwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia. Pia liliwataka wamiliki kuitoa mizigo hiyo ndani ya siku 30 kuanzia siku ilipotangazwa.

Tangazo Tangazo hilo lililotolewa na Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye lilikuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800 huku jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika bandari kavu ya DICD.
Chanzo-EATV
Share To:

Anonymous

Post A Comment: