Jeshi la Polisi limewapiga marufuku madereva bodaboda wote nchini, kubeba watoto wenye umri chini ya miaka tisa kwani kufanya hivyo ni kunahatarisha maisha ya watoto hao pamoja na kukiuka sheria za usalama barabarani.

Onyo hilo limetolewa na Kamanda Sadick Ramadhan Msangi (RTO wa Kinondoni), hii leo katika kipindi cha SUPAMIX kinachorushwa na East Africa Radio.

“Bodaboda hairuhusiwi kubeba watoto chini ya miaka tisa kwenda popote, akionekana mtu kama huyo barabarani akamatwe kwa kuwa ni kosa kisheria”, amesema Kamanda Msangi.

Aidha, Kamanda Msangi amesema changamoto kubwa ambayo wanayokumbana nayo ni kuwadhibiti madereva wa bodaboda wanaovunja sheria kutokana na kuwepo ongezeko kubwa la madereva hao kila mwaka.

“Kizazi cha waendesha pikipiki kinazaliwa kila siku, wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne kila mwaka, wengi wao wanaingia katika kazi hii. Kwa hiyo tunachofanya kwa sasa ni kwamba tukishamkamata bodaboda tunampeleka moja kwa moja kituoni na tunawaingiza darasani kuwafundisha sheria za usalama barabarani, kwa kuwa wengi wao hawajui ", ameongeza.

Mbali na hilo, Kamanda Msangi amewasisitizia madereva na raia wote kutokubali kukamatwa na askari yoyote asiyekuwa na kitambulisho, kwa madai kuwa hakuna askari anayetembea na kufanya kazi bila kitambulisho chake.

Sambamba na hilo pia amewataka raia kuripoti polisi matukio ya ajali za boda boda kwa kuchukua namba za pikipiki husika ili jeshi la polisi liweze kuwafuatilia kupitia vituo vyao wanavyoegesha pikipiki zao, badala ya kuyamaliza wenyewe.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: