Saturday, 4 August 2018

DC Kilolo atoa onyo kali baada ya Tembo kuua mtu


Na Lauson Mgani, Iringa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdala amekiagiaza kikosi cha askariv wanyamapori kuimarisha ulinzi katika tarafa ya Mahenge, wilayani kutokana na wanyamapori hasa tembo kuvamia makazi ya watu na kusababisha uharibifu wa mali za watu na vifo vya watu.

Mhe. Asia amesema hayo wakati anashiriki mazishi ya Mzee Kipapia Maramba (65) mkazi wa kitongoji cha Madaba, kijiji cha Irindi, kata ya Mahenge ambaye ameuawa kwa tembo juzi jioni wakati anarudi nyumbani akitokea msibani kijijini hapo.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilolo ambaye ameambatana na Mbunge wa Kilolo Mhe. Venance Mwamoto, amewataka maafisa wanyamapori kuhamia katika maeneo yanayosumbuliwa na tembo.

"Vijiji vya Magana, Irindi, Mahenge, Nyanzwa na Mtandika changamoto kubwa kila siku ni tembo kuvamia makazi ya watu, nyie mpo mjini mnafanya nini, nataka mhamie huku muimarishe ulinzi", alisema kwa ukali Mhe. Asia Abdala.

Akisema kwa hisia kali amesema, tukio hilo liwe la mwisho kutokea kwa uzembe wa askari wanyamapori.

" Binadamu na Wanyama, wote wanaumuhimu kwa taifa la Tanzania, hivyo lazima muweke mikakati madhubuti ya muda mfupi ya kukabiliana na tatizo hilo wakati serikali inatafuta ufumbuzi wa kudumu ikiwemo kujenga kituo cha askari wanyamapori katika kijiji cha Mtandika", alisisitiza mhe Asia.

Naye Mbunge wa Kilolo Mhe. Venance Mwamoto ambaye aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, amewataka maaskari wanyamapori kuwapa mafunzo maalumu migambo wa eneo hilo ili washirikiane nao katika suala la ulinzi.

Aidha, Mhe. Mwamoto amewashauri wakazi wa kitongoji cha Madaba ambacho kipo nje kidogo ya kijiji cha Irindi na kuzungukwa na msitu mkubwa kutundika mizinga ya nyuki kwani nyuki wanasaidia kufukuza tembo.

Aidha, amesema amewasilisha tatizo hilo kwa Waziri wa Maliasili na Utarii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangala kwa ajili ya ufumbuzi wa kudumu ambapo amewataka watafute eneo la kujenga kituo cha askari wanyapori.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtandika Bw. Mrisho Ngecha amesema kijiji chake kimekubali kutoa eneo la ujenzi wa kituo hicho.

Naye Mhifadhi Wanyamapori KDU Iringa Frank Sade amesema eneo hilo ni njia za kudumu za tembo ambazo kwa kawaida hutumika enzi na enzi kwa hiyo wananchi wanatakiwa kuchukua thahadhari, na kuahidi kuimarisha doria ili kuepusha madhara ya tembo.

Hata hivyo, wananchi vijiji vya Magana na Irindi wameshauri serikali kutatua tatizo hilo kwani limesababisha hofu kwa wananchi hivyo kushindwa kufanya kazi za uzalishaji mali kwa uhuru kwa kuhofia kuuawa kwa tembo wanaoingia kwenye makazi yao kila siku nyakati za jioni na usiku.


Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: