Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi amesema mazingira safi, afya bora ndio yanayochangia ukuaji wa maendeleo katika eneo lolote na kuwataka wananchi kuhamasishana kufanya usafi ili kwenda sawa na agizo la Rais John Magufuli la kufanya usafi.

Katambi ameyasema hayo jana wakati alipoongoza wananchi wa Dodoma Mjini kufanya usafi katika mazingira yao ikiwa ni kawaida ya wilaya hiyo kufanya usafi kila jumamosi kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli huku jumamosi ya pili ya kila mwezi ikiwa ni siku ya mazoezi.

" Mtu ni afya, usafi wa mwili na mazingira katika Jiji la Dodoma lakini pia suala la ulinzi na Usalama ni jambo la lazima, vichagizo vya uwepo wa maendeleo ni kuchapa kazi, na kazi za uzalishaji mapato hufanywa na watu wenye afya njema kwenye mazingira safi na yaliyo amani na utulivu.

" Hakuna biashara wala kazi za uzalishaji iwapo jamii itakuwa haina mazingira safi, salama na rafiki  ya kufanyia kazi, upatikanaji Kodi ni zao la shughuli za uzalishaji zinazotegemea sana mazingira  ya kazi Rais Magufuli aliliona hilo ndio maana akazindua Operation Usafi Nchi nzima na yeye kuwa mshiriki wa mara kwa mara," amesema Katambi.

Katika hatua nyingine Katambi alitumia fursa hiyo kuzungumza pia na wananchi wake na kuwataka kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na spidi ya Rais Magufuli katika kufikia Tanzania ya viwanda lakini pia alitoa nafasi kwa mwananchi yoyote ambaye anahitaji msaada wake kama Mkuu wa Wilaya kutosita kufika ofisini kwake kwani yeye ameteuliwa ili awatumikie wao hivyo wasipate hofu katika kumfikia yeye na kumueleza changamoto zao.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: