Mkuu wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo amepokea msaada wa vifaa vya usafi na vitanda vyenye thamani ya Sh5milioni vitakavyotumika katika hospitali ya wilaya hiyo.

Vifaa hivyo vimetolewa na uongozi wa Kampuni ya  Builder’s Center ya jijini Dar es Salaam.

Akipokea msaada huo leo Ijumaa Agosti 24, 2018, Jokate amesema uamuzi wa kampuni hiyo ni wa kuigwa kwa maelezo kuwa utapunguza changamoto zilizopo hospitali sambamba na kuboresha huduma za afya.

“Ninawashuruku kwa hiki mlichokifanya nawaomba mwakani mkifikiria kufanya jambo hilo, basi msiisahau Kisarawe,” amesema.

Amebainisha kuwa awali kampuni hiyo iliahidi kutoa vifaa vya usafi pekee lakini aliwaomba kuongeza na vitanda jambo ambalo walilikubali.

Ofisa masoko wa kampuni hiyo, Mussa Mondosha amesema wamechukua uamuzi huo kuunga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na changamoto ya afya.

“Tumeguswa na kuamua kutoa msaada ili kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuboresha huduma za afya. Kubwa zaidi ni kupunguza vifo vya mama na mtoto,” amesema Mandosha.

Mganga mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Dk Jonathan Budenu ametoa wito kwa jamii na kampuni mbalimbali kutoa misaada katika hospitali za Serikali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: