Saturday, 7 July 2018

Yanga kupanga mikakati ya kumpokea Manji kesho


WENYEVITI wa matawi ya Yanga kesho Jumapili watakutana na uongozi wa kwa ajili ya kupanga mikakati ya jinsi ya kumpokea aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji ambaye anatarajiwa kurudi kuendelea kuiongoza klabu hiyo.

Mei 23, mwaka jana, Manji aliyeleta mapinduzi Yanga na kuifanya timu hiyo ishiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, alitangaza kuachia ngazi ya uongozi ndani ya timu hiyo kutokana na kukabiliwa na matatizo mbalimbali yakiwemo ya kiafya.

Hivi karibuni wanachama hao kwa pamoja katika mkutano wao mkuu waligoma kuridhia uamuzi huo wa Manji wa kujiuzulu na kudai kuwa bado wanamtambua kama mwenyekiti wao mpaka mwaka 2020 ambapo muda wake wa uongozi utamalizika hivyo wakautaka uongozi wa klabu hiyo kumpatia taarifa juu ya maamuzi yao hayo.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba, baada ya uongozi kupokea majibu kutoka kwa Manji kuhusiana na maamuzi ya wanachama wa klabu hiyo kugomea kujiuzulu umepanga kufanya mkutano wa kujadili kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar.

“Hivi karibuni tumepokea ujumbe wa mwenyekiti wetu Manji kutokana na barua tuliyompelekea kuhusiana na maamuzi ya mkutano mkuu uliofanyika hivi karibuni ambapo wanachama wote waligomea suala la kujiuzulu kwake.

“Ujumbe huo ni mzuri na umefufua matumaini yetu yaliyokuwa yamepotea hapo awali, kwa hiyo Jumapili tutakutana na viongozi wa matawi kwa ajili ya kupanga mikakati ya jinsi ya kumpokea upya kiongozi wetu huyo,” kilisema chanzo cha habari.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa ili aweze kuzungumzia hilo hakupatikana lakini ofisa habari wa klabu hiyo, Dismas Ten alithibitisha kuwepo kwa mkutano huo huku akidai hafahamu unahusu nini.

No comments:

Post a Comment