Friday, 13 July 2018

Waziri wa Afya azindua mradi wa TUWATUMIE Itilima mkoani Simiyu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amezindua rasmi mradi wa TUWATUMIE unaotekelezwa katika wilaya za Itilima mkoani Simiyu na Misungwi mkoani Mwanza. 

 Uzinduzi wa mradi huo unaotekelezwa na shirika la Amref Health Africa Tanzania pamoja na taasisi ya Benjamin Mkapa umefanyika katika wilaya ya Itilima, ukilenga kuboresha huduma za afya hususani huduma za uzazi ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto chini ya miaka mitano. 

 Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri Mwalimu amesema serikali itaendelea kuboresha huduma za afya ikiwemo kuongeza watumishi wa afya pamoja na kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili wasaidia kutoa huduma za afya kwa wananchi. Naye Mkuu wa Miradi kutoka shirika la Amref Health Africa Tanzania, Dkt.Aisa Muya amesema utekelezaji wa mradi wa TUWATUMIE unaofadhiliwa na serikali ya Ireland kupitia shirika la Irish Aid, ulianza mwezi Disemba 2017 na unatarajiwa kufikia tamati mwezi Juni mwaka 2020 ambapo ametoa rai kwa serikali kuandaa mwongozo utakaowaajiri wasaidizi hao wa afya ngazi ya jamii baada ya kipindi cha mwaka mmoja ambacho shirika hilo litakuwa likiwalipa mishahara kukamilika.

 Amesema mradi huo ulibuniwa na shirika la Amref Health Africa Tanzania kwa kushirikiana na taasisi ya Benjamin Mkapa pamoja na Wizara ya Afya kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma (Health Promotion Unit) lengo likiwa ni kuajiri watumishi wapatao 215 wilaya za Itilima na Misungwi (Itilima wahudumu 102 na Misungwi wahudumu 113) ili wasaidie utoaji huduma za awali kwa wananchi. 

 “Asilimia 50 ya miradi yetu inatumia watoa huduma za afya ngazi ya jamii ambapo kwa mwaka huu tayari wahudumu 2,265 wamepatiwa mafunzo na majukumu yao makubwa yanaanza kwa kuwahamasisha wananchi kuzingatia usafi wa mazingira, utumiaji wa maji safi na salama, kuzuia ukatili wa kijinsia, kutoa elimu ya lishe bora, kutambua viashiria vya magonjwa hatarishi kwa akina mama”. 

Amesema Dr.Muya. Nao baadhi ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii wilayani Itilima wamesema wako tayari kufanya kazi kwa bidii na weledi hususani kuwahamasisha wananchi kuhudhuria kliniki, kujifungulia katika vituo vya afya ili lengo la kupunguza vifo vya akina mama na watoto chini ya miaka mitano liweze kutimia.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto akiongea na Wananchi wa Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu wakati wa ufunguzi wa mradi wa Tuwatumie ambao unawaajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika vijiji vyote vya halmashauri hiyo chini ya ufadhili wa AMREF
Waziri Ummy Mwalimu akifungua mradi huo
Wadau mbalimbali wa sekta ya afya walifuatilia hotuba ya mgeni rasmi(hayupo pichani) aliyekaa kushoto ni Niall Morris Mkuu wa Arish Aid,Dar.Aisa Muya -Kaimu Mkurugenzi Mkazi Amref Tanzania(katikati) na kulia ni Dkt.Helen Senkoro Mkurugenzi wa Benjamin Mkapa Foundation
wananchi waliojitokeza kushuhudia ufunguzi wa mradi huo ambapo watoa huduma hao watakua kiungo kati ya wananchi na vituo vya kutolea huduma

No comments:

Post a Comment