Friday, 13 July 2018

Waziri Ummy atoa agizo baada ya gari la wagonjwa kukamatwa na Mirungi


Ikiwa ni siku mbili baada ya kukamatwa kwa gari ya kubebea Wagonjwa (Ambulance) ya Hospitali ya Wilaya ya Tarime ikiwa imebeba Kilo 800 za Dawa za Kulevya aina ya Mirungi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameibuka na kulizungumzia suala hilo.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu katika ufunguzi wa mradi wa ‘Tuwatumie’ unaohusisha watoa huduma za afya ngazi ya jamii amekemea vikali magari ya wagonjwa kubeba dawa za kulevya na vitu vingine tofauti na wagonjwa na ametoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime kumsimamisha kazi mara moja dereva wa Ambulance iliyotumika kubebea Dawa hizo za kulevya pamoja na wote waliohusika.

“Ninakemea jambo hili kwa nguvu zangu zote na nawataka waganga wakuu wa mikoa na Wilaya kote nchini kusimamia matumizi ya magari ya kubebea wagonjwa” Waziri Ummy

“Ni marufuku gari tofauti la kubeba wagonjwa kubeba kitu tofauti na mgonjwa, yoyote ambye tumemkabidhi gari la kubebea wagonjwa tutamchukulia hatua kali pale ambapo atakiuka muongozo wa matumizi ya gari la kubebea wagonjwa,” amesema Waziri Ummy.

Pamoja na hatua alizochukua Mwalimu amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara kwa kuchukua hatua ya kukamata gari hiyo iliyobeba dawa za kulevya.

No comments:

Post a Comment