Saturday, 7 July 2018

Waziri Jafoo Atoa Agizo Kwa Wakuu Wa Mikoa Wote Nchini

Na  Stella Kalinga, Simiyu
Waziri wa Nchi  Ofisi ya Rais   Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR-TAMISEMI) Mhe.Selemani  Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa nchini kuweka mpango mkakati wa kuwahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulioboreshwa kama alivyofanya  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka, ili kuwapunguzia wananchi gharama za matibabu.

Mhe. Jafo alitoa agizo hilo wilayani Busega mkoani Simiyu katika hafla ya kupokea Majengo ya wodi ya wazazi na chumba cha upasuaji  katika Kituo cha Afya NASA, ikiwa ni moja ya vituo vya Afya 38 mkoani Simiyu, pamoja na magari tisa yakiwepo magari matatu ya kubebea wagonjwa (Ambulance) na magari Sita kwa ajili ya uratibu wa huduma za Afya  yaliyopatikana chini ya ufadhili wa  UNFPA/KOICA , msaada uliogharimu jumla ya shilingi bilioni 5.52.

 “Agenda yako Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ya kuhakikisha wananchi wote wanajiunga na Bima ya Afya, wewe utakuwa Mkuu wa Mkoa Kinara ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia mkutano huu niwaagize wakuu wa mikoa wote wahakikishe wanakuja na mpango wa kuwasaidia wananchi wao kupitia mikakati  watakayoibuni, kuwa kila mwananchi anakuwa na bima ya afya kupitia CHF iliyoboreshwa” alisema Jafo.

Awali akikagua  jengo la wodi ya wazazi na jengo la upasuaji katika kituo cha Nasa Waziri Jafo amepongeza viongozi wa Wilaya ya Busega na Mkoa wa Simiyu kwa kusimamia na kuhakikisha majengo hayo yanajengwa katika viwango bora kwa kutumia “Force Account” na kuwataka wananchi kuyalinda na kuyatunza majengo hayo.

Mhe. Jafo amewataka Waganga  Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanatoa huduma za afya vizuri katika maeneo yao kwa kuhakikisha kuwa wanakagua vituo vyao mara kwa mara badala ya kukaa ofisini.

Aidha, amewataka kuboresha mazingira ya vituo vyote vya afya nchini kuhakikisha vinakuwa visafi, huku akisisitiza  kusimamia kufungwa kwa mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato,   ili kuhakikisha kuwa mapato hayapotei.

Mhe. Jafo, amewataka wataalamu wa afya kuhakikisha wanakusanya na kuwa na takwimu sahihi za watoto wanaozaliwa na kufariki ili kuwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi zitakazowezesha kupambanana tatizo  la vifo vya akina mama na watoto.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Anthony Mtaka amewashukuru wafadhili Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA), kwa namna walivyoshirikiana na Serikali katika kuchangia kuboresha huduma za afya mkoani humo, ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya kutolea huduma za afya.

Kuhusu mkakati wa Mkoa juu ya Bima ya Afya, Mtaka amesema “Tungehitaji kuwa ni mkoa ambao kila mwananchi atafaidika na huduma zinazotolewa na  Hospitali na vituo vingine vya kutolea huduma za afya kwa kuwa na bima ya afya ili waweze kupata matibabu yao vizuri” .

Naye, Mkuu wa Idara ya Afya KOICA Tanzania  Kira Thomas amesema pamoja na kufadhili ujenzi wa vituo vya afya mkoani Simiyu, mkakati wao ni kuhakikisha Zahanati 31 mkoani Simiyu zinapatiwa vifaa vya dharura kwa ajili ya kutoa  huduma za dharura na kuongeza  damu kwa mama wajamzito wakati wa kujifungua.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Busega Mbunge wa Jimbo la Busega Dkt. Raphael Chegeni amesema uwepo wa wodi ya wazazi na chumba cha upasuaji utatatua changamoto ya huduma za afya ya muda ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma na akaishukuru Serikali kwa kutenga shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya.

No comments:

Post a Comment