Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi akimpa kitambulisho mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya Polisi Jamii wa Mtaa wa Kanisani kata ya Sokoni One jijini Arusha.
Meya wa Jiji la Arusha Bw. Kalist Lazaro akiongea na wananchi wa mtaa wa Kanisani kata ya Sokoni One kabla Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha kufunga rasmi mafunzo ya kikundi cha ulinzi shirikishi cha mtaa huo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi pamoja na wageni wengine wakiwa katika picha ya pamoja na askari wa kikundi cha Ulinzi Shirikishi cha Mtaa wa Kanisani kata ya Sokoni One kilichopo jijini Arusha. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha).

Na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha

Wananchi wa mtaa wa Kanisani kata ya Sokoni One jijini hapa, wametakiwa kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao na kikundi cha ulinzi shirikishi ili kuweza kuimarisha usalama katika eneo lao.

Wito huo ulitolewa jana jioni na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi wakati alipokuwa anafunga mafunzo ya wiki mbili ya kikundi cha ulinzi shirikishi cha mtaa huo pamoja na kuwapa vitambulisho askari 16 waliopewa mafunzo hayo.

Kamanda Ng’anzi alisema mbali na askari wa kikundi hicho kufanya doria katika eneo hilo pia watahitaji kupata taarifa za uhalifu toka kwa wananchi ili waweze kubaini maeneo korofi ambapo kama zitakuwa juu ya uwezo wao watashirikiana na Jeshi la Polisi.

Aidha aliwataka askari hao kufanya kazi kwa kufuata taratibu kama jinsi walivyoelekezwa katika mafunzo yao na kutomuonea mtu yoyote hali ambayo itasidia kuimarisha mahusiano bora baina yao na wananchi.

Hata hivyoKamanda Ng’anzi  aliwataka wananchi hao nao pia wawe mstari wa mbele katika jukumu la ulinzi badala ya kutegemea baadhi ya vyombo vya ulinzi pekee kwani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewapa dhamana.

Naye Meya wa jiji la Arusha ambaye pia ni Diwani wa kata ya Sokoni One Bw. Kalist Lazaro aliahidi kuendeleza ushirikiano kati ya halmashauri ya jiji na Jeshi hilo katika masuala ya usalama.

Alisema askari wa Jeshi la Polisi hawawezi kuenea kila mtaa bali wananchi wanatakiwa watoe michango yao kwa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi kama wa mtaa wa Kanisani walivyofanya na kuongeza kwamba endapo kila mtaa utaanzisha vikundi hivi basi hali ya usalama jijini hapa itazidi kuimarika zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Polisi Jamii mkoa wa Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Edith Makweli alisema kwamba, mpaka hivi sasa mkoa wa Arusha una jumla ya vikundi vya Ulinzi Shirikishi 147 ambavyo vimeweza kushirikiana na Jeshi la Polisi na kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa ambapo mwaka 2016 uhalifu ulipungua kwa asilimia 6.8 na mwaka 2017 uhalifu ulipungua kwa asilimia 17.9 ikilinganishwa na mwaka 2016.

Uwepo wa kikundi hicho chenye zaidi ya miaka 11 katika mtaa huo umeleta amani kwa wakazi hao kwani awali matukio ya uhalifu yalikuwa yanatokea mara kwa mara katika barabara kuu ya mtaa huo tofauti na sasa hali iliyomlazimu Paroko Reginald Kimati wa Kanisa ya Parokia ya Vicent Paroti apendekeze iitwe Amani road.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: