Friday, 13 July 2018

Wakili afungua kesi akihoji matokeo ya urais kutopingwa mahakamani

Wakili wa kujitegemea jijini Dar es Salaam, Jebra Kambole amefungua kesi katika Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu (AfCHPR), akiiomba iamuru matokeo ya urais nchini yapingwe mahakamani.

Kambole aliwasilisha maombi ya kufungua kesi hiyo katika mahakama hiyo Julai 4 na juzi ilimwandikia barua kumtaarifu kuwa imepokea maombi yake na kuyasajili kwa namba 018 ya mwaka 2018.

Naibu msajili wa mahakama hiyo, Nouhou Diallo alithibitisha jana kupokewa na kusajiliwa kesi hiyo.

Katika maombi hayo dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kambole anapinga ibara ya 41 (7) ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977 inayozuia matokeo ya urais yakishatangazwa kupingwa mahakamani.

Ibara hiyo inasomeka, “Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”

Kambole anadai kitendo cha Serikali kuruhusu Katiba yenye ibara inayozuia mtu asiyeridhika na matokeo ya urais kuyapinga mahakamani kinakiuka ibara za 1, 2, 3 (2) na 7(1) (a) za Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu.

Anadai Serikali imeshindwa kutekeleza wajibu wake chini ya mkataba huo wa Afrika kama mwanachama wa Umoja wa Afrika, kutambua haki, wajibu na uhuru unaolindwa na mkataba na kuchukua hatua kulinda haki hizo.

Kambole anasema Tanzania ilipata uhuru mwaka 1961 na ni nchi mwanachama wa Umoja wa Afrika ikiwa mshirika katika Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu.

Anadai ukiukwaji anaoulalamikia wa haki ambazo zinalindwa na mkataba hadi sasa unaendelea kutokea katika mipaka ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anaiomba mahakama iamuru kwamba Serikali inakiuka ibara ya 1, 2, 3(2) na 7(1) ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na iweke kwenye Katiba na sheria hatua za kuhakikisha haki zinazotolewa katika mkataba huo zinalindwa.

Pia, anaiomba mahakama iiamuru Serikali kutoa taarifa mahakamani hapo ndani ya miezi 12 tangu kutolewa kwa hukumu, kuhusu hatua za utekelezaji wa hukumu na matokeo ya amri za mahakama.

No comments:

Post a Comment