Dereva wa gari la kubeba wagonjwa (ambulance) ashikiliwa na polisi baada ya gari alilokuwa akiendesha kukamatwa likiwa na shehena ya mirungi.

Tukio hilo limetokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mara, ambapo leo, Julai 11, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema gari hilo lilikamatwa jana Julai 10, wilayani Bunda.

Malima amesema dereva huyo alitakiwa kumsafirisha mgonjwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

"Dereva wa gari hilo aliitwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kubeba mgonjwa usiku wa jana lakini alisema yupo mbali na gari halina mafuta,” amesema Malima.

Akifafanua zaidi Malima amesema baada ya dereva kutoa udhuru, mgonjwa aliyehitaji huduma ya rufaa alisafirishwa kwa kutumia gari la polisi.

“Lakini gari la polisi likiwa njiani kuelekea jijini Mwanza, waliokuwamo ndani ya gari hilo waliiona ‘ambulance’ inayodaiwa kutokuwa na mafuta ikiwa eneo la Bunda.”

"Askari polisi na maofisa wengine waliokuwamo kwenye gari la polisi walilazimika kulisimamisha lile gari la wagonjwa kujua lilikotoka na linakoelekea ndipo wakamkuta dereva ambaye awali alidai gari halina mafuta ndipo walipokuta limesheheni shehena la mirungi,” amesema

Amesema dereva yule hakuwa na la kujitetea ndipo alipotiwa mbaroni na anaendelea kushikiliwa kwa mahojiano,"

Mkuu huyo wa mkoa amesema taarifa zaidi kuhusu tukio hilo la aina yake kuwahi kutokea mkoani Mara zitatolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: