Sunday, 8 July 2018

Rais Magufuli Kampa Ujumbe Mzito Balozi wa Marekani....." Wambie Boeing Wakamilishe Haraka Ndege Yetu ya Pili, Pesa Ipo"

Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemtaka Balozi wa Marekani afikishe salamu zake kwenye Kampuni ya ndege ya Boeing kuwa wakamilishe haraka ndege ya pili inayotakiwa kufika Tanzania kwa kuwa hela za kulipia zipo.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo  katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, wakati wa sherehe za kupokea ndege mpya ya Boeing 787-8 Dreamliner  iliyowasili leo kutokea Seattle nchini Marekani.

"Ndege hizi ni matokeo ya Watanzania kulipa kodi na kuchapakazi. Nawapongeza wote walioshiriki kikamilifu. Ndege zote hizi tumenunua kwa fedha zetu wenyewe, hatujakopa kwa mtu. Tunataka Balozi wa Marekani utufikishie salam Boeing kuwa ile Dreamliner ya pili waikamilishe haraka, hela tunazo" - Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameongeza kwamba "Madai kuwa Watanzania wengi  hawafaidiki na ndege hayana msingi. Wapo wengi wanaohitaji ndege bei ilikuwa juu. Ndege hii imewafurahisha wengi na kama yupo mtu hajafurahia tukio hili basi huyo atapata tabu sana!-Rais Magufuli

Pamoja na hayo Rais amefafanua kuwa ndege hiyo imeletwa ili iweze kuimarisha na kuongeza mapato ya utalii nchini kwa kuwa 70% ya watalii wanatumia ndege.

Mh. Rais amesisitiza kwamba "Ukiongeza ndege wasafiri wanaongezeka. ATCL imeongeza wasafiri kutoka 4000 kwa mwezi mpaka 21,000 kwa mwezi. Tunaboresha usafiri wa reli, majini na barabara. Waliodhani kuwa maboresho ya Bandari hayana tija sasa wameaibika".

No comments:

Post a Comment