Wagombea 30 wa Udiwani katika uchaguzi Mdogo wa kata 77 utakaofanyika Agosti 12 mwaka huu, wamepita bila kupingwa. 

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Athumani Kihamia amesema kuwa wagombea hao wamepita bila kupingwa baada ya Tume kukutana, kujadili na kuyatolea maamuzi mapingamizi mbalimbali yaliyoweka na wagombea wa udiwani.

 Amesema Madiwani wote waliopita bila kupingwa wanatoka Chama cha Mapindizi (CCM) na kuongeza kuwa rufaa zilipokelewa na kujadiliwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 44(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kikisomwa pamoja na Kanuni ya 28(1)(2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015.

“Tume, ilipokea, ilijadili na kufanya maamuzi ya Rufaa 25 ambapo jumla ya wagombea kumi (10) walifanikiwa na hivyo kuendelea na uchaguzi na wagombea 15 rufaa zao hazikufanikiwa na hivyo kutoendelea kuwa wagombea,” amesema Dkt. Kihamia.

Ameongeza kuwa katika kata sabini na saba (77) wanachama 254 kutoka vyama kumi na moja (11) vya siasa walichukua fomu za uteuzi na kwamba jumla ya wanachama 186 sawa na asilimia 73.2 ya waliochukua fomu za uteuzi walizirejesha na kuteuliwa kuwa wagombea ambapo kati yao wagombea 179 sawa na asilimia 96.2 ni wanaume na wagombea 7 sawa na asilimia 3.8  ni wanawake.

“Hadi muda wa mwisho wa uteuzi ulipofika (saa 10.00 jioni siku ya uteuzi)  wanachama 68 sawa na asilimia 26.8 ya waliochukua fomu hawakuteuliwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kutorudisha fomu, kurudisha fomu nje ya muda unaokubalika kisheria na fomu kutojazwa ipasavyo,” amesema.

Dkt. Kihamia amefafanua kuwa katika uchaguzi huu mdogo wa madiwani utakaofanyika Agosti 12 mwaka huu jumla ya vyama kumi na moja (11) vimesimamisha wagombea.

Amewataja Wagombea hao katika Kata kwa kila Chama kuwa ni ACT-Wazalendo Wagombea 17 (sawa na asilimia 22), ADC Wagombea 3 (sawa na asilimia 3.9), CCM Wagombea 77 (sawa na asilimia 100) CHADEMA Wagombea 54 (sawa na asilimia 70), CHAUMMA Wagombea 2 (sawa na asilimia 2.6), CUF Wagombea 17 (sawa na asilimia 22), Demokrasia Makini Wagombea 4 (sawa na asilimia 5.2), NCCR-MAGEUZI Wagombea 6 (sawa na asilimia 8), NRA Wagombea 3 (sawa na asilimia 3.9), SAU Mgombea 1 (sawa na asilimia 1) na UPDP Wagombea 2 (sawa na asilimia 2.6).

Wakati huohuo, Dkt. Kihamia amesema kwamba katika jimbo la Buyungu jumla ya wanachama kumi (10) kutoka vyama kumi (10) vya siasa vya AAFP, ACT-Wazalendo, CCM, CHADEMA, CUF, DP, Demokrasia Makini, NRA, UMD na UPDP walichukua fomu za uteuzi.

 “Wanachama wote kutoka vyama hivyo walirejesha fomu na kuteuliwa kuwa wagombea wa Ubunge katika Jimbo hilo, kati yao wanaume ni tisa (9) na mwanamke mmoja (1),” amesema Dkt. Kihamia.

Amevitaka vyama vya siasa na wagombea wao kuzingatia maadili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015, wakati wote wa kampeni na siku ya uchaguzi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: