Na WAMJW Shinyanga
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kufuata vipaumbele vya Serikali katika maeneo wanayofanya kazi na kutoa huduma .

Ameyasema hayo mkoani Shinyanga wakati akizungumza na wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga wakuu wa Wilaya na Maafisa Maendeleo ya Ustawi wa Jamii katika hitimisho la ziara yake mkoani humo.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini ni wadau muhimu katika Maendeleo ya taifa ila wanapaswa kufuata vipaumbele vinavyotolewa na Mikoa na Halmashauri wanazoenda kufanya kazi na kutoa huduma.

Ameongeza kuwa katika Mikoa mingi kumekuwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayofanya kazi za aina moja kwa watu wa aina moja hivyo kufanya maeneno mengine kukosa nguvu.

Ametolea mfano changamoto iliyopo ya mimba na ndoa za utotoni katika baadhi ya Mikoa ukiwemo mkoa wa Shinyanga hivyo wadau wanapaswa kuelekeza nguvu katika kupambana na masuala muhimu ya eneo husika.

“Niwapongeze wadau wetu ila pia niwaase tu tuzingatie vipaumbele vya Mikoa na Halmashauri ili kusaidiana na Serikali katika Maendeleo” alisisitiza Dkt. Ndugulile

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Josephine Matiro amemuhakikishia Naibu Waziri  kuwa watasimamia kwa kuratibu kwa  karibu kazi zote zinazofanywa na wadau.

“Nikuhakikishie Mhe. Naibu Waziri tulisimamia agizo lako kwa ukamilifi” alisema Mhe. Josephine.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: