Mwapulise Mwafikwa (28) anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji ambaye alitoroka akiwa chini ya ulinzi katika mahakama ya Wilaya ya Njombe mkoani Njombe amekamatwa na polisi mkoani Dodoma.

Mwafikwa anakabiliwa na kesi ya mauaji namba PI 08/2015 ambapo pia anadaiwa aliwahi kufungwa jela kwa kosa la kupatikana na silaha.

Akizungumza leo Alhamisi Julai 26, 2018 kamanda wa polisi mkoani Dodoma, Gilles Muroto amewaeleza waandishi wa habari kuwa mshatakiwa huyo alikamatwa Julai 24, 2018.

Amesema baada ya kutoroka alijificha katika mashamba Kiteto Mkoani Manyara na katika kiijiji cha Ngomai Wilaya ya Kongwa.

Kamanda Muroto amesema kuwa mshtakiwa huyo atasafirishwa kwenda Wilayani Njombe ili kuendelea na kesi yake ya mauaji pamoja na kufunguliwa shtaka la kutoroka akiwa chini ya ulinzi.

“Kwa kuwa taarifa za kutoroka kwake zilienea maeneo mengi mkoani hapa watu wema wasiopenda uhalifu walifanikisha kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha kituo cha polisi Kibaigwa,”amesema.

“Nawapongeza wananchi waliofanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyu hatari, niwaombe waendelee kutoa ushirikiano kwa polisi.”
Share To:

msumbanews

Post A Comment: