Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Lumumba, Dar es Salaam
13 Julai 2018

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa watanzania kuwa tarehe 17-18 Julai 2018 kutafanyika Mkutano wa Kidunia wa Vyama vya Siasa, Kikao Maalum cha Afrika, Jijini Dar es Salaam. Mkutano huu utaleta zaidi ya vyama vya siasa 38 kutoka Afrika na zaidi ya washiriki 130 kutoka nje ya Afrika. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepata heshima kubwa kuwa mwenyeji wa Mkutano huu wa kidunia.

Mkutano huu umeandaliwa kwa ushirikiano wa Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkutano huu ni sehemu ya matokeo mazuri ya utendaji kazi wa uongozi wa awamu ya tano ya Chama na Serikali chini ya Ndg. John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkutano huu wa kihistoria na wa kwanza kufanyika Barani Afrika ni wapili kufanyika baada ya Mkutano kama huu wa kidunia kufanyika Jijini Beijing, China Mwezi Disemba mwaka 2017. Mkutano wa mwezi Disemba 2017 uliandaliwa na Chama Cha Kikomunisti Cha watu China (CPC) na Kiongozi Mwenyeji wa Mkutano huu alikuwa ni Kamaradi Xi Jinping Katibu Mkuu wa CPC na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China.

Mkutano huu wa utahudhuriwa pamoja na wajumbe wengine wa mkutano ni Kamaradi Song Tao Waziri wa Mambo ya Nje wa Chama Cha Kikomunisti cha Watu wa China, Kamaradi Xu Luping Makamu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Chama Cha Kikomunisti cha China na Kiongozi Mwenyeji wa Mkutano huu wa Kidunia wa Vyama vya Siasa ni Kamaradi John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wazo la Mkutano huu wa kidunia linatokana na fikra za Kamaradi Xi Jinping Katibu Mkuu wa CPC na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China ambaye anapendekeza fikra ya mwelekeo mpya wa namna tunaenenda kidunia kwamba, “tushirikiane kujenga jamii ambayo ina matarajio ya pamoja ya baadaye na kufanya kazi pamoja ili kujenga Dunia bora”. Fikra hizi za Kamaradi Xi ndio zilizopelekea majadiliano ya kidunia kati ya CPC na Vyama vya Siasa vya Kidunia.

Mwaka huu Nchi ya China inatimiza miaka 40 ya kufanya Mageuzi na Kuchangamana Kimataifa na Mkutano huu wa Dar es Salaam utakuwa hatua kuelekea katika Kongamano kubwa la ushirikiano wa China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation – FOCAC) litakalofanyika jijini Beijing, China. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba Tanzania, Afrika na China katika Mkutano huu watajikita katika mjadala mpana na wa kina wa kuziangazia changamoto na fursa lukuki zitokanazo na kujengeka zaidi kwa mahusiano na mashirikiano ya Afrika na China.

Jambo moja ambalo lina mfanano mkubwa kati ya China na Tanzania na CCM na CPC ni itikadi ambayo inatoa mwelekeo wa Sera za China na Tanzania. Mataifa haya mawili na vyama viwili ambayo ndio vinatoa uongozi katika nchi hizi mbili zinaamini katika Itikadi ya Ujamaa. China imeongozwa kwa mafanikio kwa zaidi ya miaka 40 sasa na Siasa na Itikadi ya Ujamaa wa Kisayansi ambao unashajihishwa na tabia ya Taifa la China “Socialism with Chinese characteristics”. Itikadi hii ya Ujamaa ndio imewezesha mafanikio ya Mageuzi na Mapinduzi makubwa ya kimfumo, kiutendaji, kiuongozi, kiuchumi na kisiasa ambayo Taifa la China limeyatenda katika kipindi hiki za miaka 40.

Wakati huu China imeanza awamu mpya ya Mageuzi na Mtangamano wa Kimataifa na inaweka jitihada kubwa kufikia lengo la kujenga Taifa la kijamaa la kisasa na imara ifikapo mwaka 2050. Wakati China inaweka malengo haya makubwa ifahamike kwamba Bara la Afrika likiwa mojawapo ya mabara yanayokua haraka kiuchumi, kwa idadi ya watu, kwa utangamano na uwezekano mkubwa wa uchumi wake kukua kwa faida na tija duniani; Afrika pia imejitoa kuhakikisha inafikia Mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kujitengenezea njia yake ya kukua kulingana na mazingira ya Afrika “exploring independent path of modernisation”.

Katika njia hii ya pamoja kuelekea katika lengo la pamoja na kwa lugha rahisi “kushughulika na shida za watu wetu”, CPC iko tayari kuimarisha utaratibu wa kubadilishana taarifa, maarifa na watu pamoja na vyama vya siasa vya Afrika ili kujenga jamii ya pamoja ya Afrika na China na yenye lengo la pamoja kuhusu maisha bora ya sasa na ya baadaye kwa watu wetu.

Mada kuu ya Mkutano huu wa kidunia itakuwa ni Juhudi (vitendo) na Nadharia za Vyama vya Afrika na Chama Cha Kikomunisti cha China katika kufanya uchaguzi wa njia sahihi za kujiletea maendeleo na zinazoendana na mazingira ya nchi zetu za Afrika.

Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Kikomunisti Cha China na vyama vyote vitakavyoshiriki katika Mkutano huu wa kidunia vitakuwa na majadiliano ya kina na ya kweli na kubadilisha taarifa na maarifa mbalimbali. Baadhi ya mada ndogo zitakazojadiliwa ni pamoja na “Majukumu ya kimaendeleo na machaguo ya njia za kujiletea maendeleo kwa China na Afrika”, “Fursa zilizopo na Changamoto za Mashirikiano ya Afrika na China” na “Wajibu wa vyama vya siasa katika ujenzi wa maendeleo ya kitaifa na mashirikiano baina ya China na Afrika”.

Mada zote hizi zinalenga kutupa hamasa katika jitihada zetu Afrika na China katika kuchagua njia sahihi za kukua, kujiletea maendeleo, kupendekeza programu ya vyama vya siasa kwa Kongamano la Ushirikiano wa China na Afrika litakalofanyika Jijini Beijing na kujenga uelewa wa pamoja na kuweka mchango wa hoja katika Ubia wa Kimkakati kati ya Afrika na China na hasa katika kipindi hiki kipya.

Mkutano huu utakuwa fursa kubwa kwa Tanzania kukumbusha na kusisitiza msimamo wake katika diplomasia ya kisiasa na kiuchumi na hasa katika zama hizi za uongozi wa awamu ya tano ambayo imejikita katika kutimiza wajibu wa kizazi cha sasa wa kulikomboa bara la Afrika na Tanzania Kiuchumi ili kuleta maendeleo ya haraka kwa watu wake wa Tanzania na Afrika.

Ifahamike kwamba tangu uongozi wa awamu ya tano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali umejikita katika kushughulika na shida za watu kwa kuimarisha nyanja zote za kiuchumi na kijamii. Hii imekwenda sambamba na kuimarisha nidhamu ya viongozi na watumishi wa umma, kuweka nidhamu katika makusanyo na matumizi ya fedha za umma, kuongeza uaminifu, uadilifu, uchapa kazi, kuongeza mapambano dhidi ya rushwa na vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma na uhujumu uchumi.

Chama cha CPC na Serikali ya China imevutiwa sana na mwelekeo huu wa Tanzania chini ya Kamaradi John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni Imani yetu yetu kwamba Tanzania itanufaika kwa muda mfupi wakati wa mkutano huu kwa kutoa huduma mbalimbali kwa wageni hawa lakini pia itanufaika maradufu kwa matokea ya Mkutano huu na mwendelezo wake.
 

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
 
Imetolewa na,
 
HUMPHREY POLEPOLE

KATIBU WA NEC – ITIKADI NA UENEZI
Share To:

msumbanews

Post A Comment: