Jeshi la polisi mkoani Geita linawashikilia madereva wawili wa kampuni ya mabasi ya King Msukuma kwa makosa ya kuendesha magari yakiwa mabovu na kuhatarisha usalama wa abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Mwanza kwenda Kagera na jingine likitokea Kagera kwenda Mwanza.

Ubovu wa magari hayo ulisababisha abiria 120 kulazimika kulala kwenye kituo kikuu cha polisi Geita hadi walipoletewa usafiri mwingine jana asubuhi na kuendelea na safari zao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 3, Kamanda wa polisi mkoani hapa Mponjoli Mwabulambo amesema magari hayo yalikamatwa jana saa 11 jioni katika operesheni ya ukaguzi wa magari inayoendelea mkoani hapa.

Mponjoli amesema katika operesheni waliyoifanya walikagua magari 59 na 47 yalikutwa na makosa madogomadogo na kutozwa faini, mawili yalikuwa na matatizo makubwa na kuzuiwa kuondoka huku mengine yakiruhusiwa kuendelea na safari baada ya kuonekana hayana tatizo.

Amesema madereva wa mabasi ya kampuni ya King Msukuma wanaoshikiliwa ni Kini Daud (50) na Omary Oloyce.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: