Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, amewasimamisha kazi Maofisa na Askari Wanyamapori wote 27 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, TAWA ,katika Pori la Akiba Uwanda akiwemo Kaimu Meneja, Lackson Mwamezi kwa kushindwa kusimamia vizuri pori hilo.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku tatu tangu amsimamishe kazi Meneja wa Pori hilo, Mark Chuwa kwa tuhuma kama hizo pamoja na tuhuma nyingine ikiwemo kushindwa kuondoa ngo'mbe zaidi ya 12,000 ambao wamedaiwa kuwepo ndani ya pori hilo.

Amefafanua kwamba, tuhuma hizo kuwa ni pamoja na kudaiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wavuvi wanaovua samaki Ziwa Rukwa kwa kuwatoza kila mmoja Shilingi 100,000 kwa mwezi na kuruhusu mifugo kuchungwa hifadhini kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo kila mfugaji hutozwa kati ya Shilingi milioni sita hadi saba.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ametoa siku 30 kwa wananchi wote wenye mifugo ndani ya pori hilo kuitoa kwa hiari yao wenyewe kabla ya operesheni maalum itakayowaondoa kwa nguvu.

Pori la Akiba Uwanda lipo katika Bonde la Ziwa Rukwa katika Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa na linasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, TAWA.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: