Monday, 16 July 2018

KANISA lagawa Pikipiki kwa wachungaji,Polisi

KANISA la Pentecostal Assemblies of God (PAG), limegawa Pikipiki kwa wachungaji wake ikiwamo Kituo cha Polisi cha wilaya ya Hanang mkoani Manyara. 

Lengo la kutolewa kwa vyombo hivyo vya usafiri ni kuwawezesha Wachungaji hao kuwafikia watu wengi hususani wanaoishi pembezoni pamoja na kuunga mkono juhudi za jeshi la polisi katika kupambana na uhalifu. 

Akizungumza wakati wa Ibada fupi ya kuzindua pikipiki pamoja na kumuombea Rais Dk.n Magufuli iliyofanyia Kanisa la PAG Hanang’ Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Daniel Awet, aliwataka kutumia pikipiki hizo kuhubiri Injili ya Yesu ili jamii inayowazunguka iache matendo ya maovu. 

“Tumieni Pikipiki hizi kama nyenzo ili Injili ifike kwa kasi kwa waamini hasa maeneo ambayo mlikuwa hamuwezi kufika lakini sasa mmepata nyenzo za kuwafikisha,” alisema Askofu Awet. Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Polisi wilaya ya Hanang’, Sutibert Tryphone, alisema pikipiki waliyopewa itawasaidia kuhudumia wananchi mpaka kwenye maeneo ambayo magari hayafika. 

“Maeneo mengi ambayo hayapitiki kwa usafiri wa magari, sasa tutakuwa tunatumia pikipiki, tunaomba wadau wengine nao wajitokeze kutuunga mkono,” alisema OCD Tryphone. Naye Mchungaji Alex Mapanga wa PAG, ambaye kampuni yake iliwezesha kuagiza pikipiki hizo toka kiwandani kwa fedha zilichangwa na waamini wa kanisa hilo, alisema ataendelea kushirikiana na waamini katika kukfanikisha upatikanaji wa usafiri kwa wachungaji. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Hanang’ Mary Nagu, aliliomba kanisa hilo kuendelea kuliombea amani taifa na Rais John Magufuli. “Amani na utulivu ziwafanye mchape kazi ndani ya kanisa, serikalini na kwa jamii,” alisema na kuongeza, kanisa hilo limefanya jambo jema kuwawezesha wachungaji wake kupata vyombo vya usafiri.


Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentecostal Assembilies of God (PAG), Daniel Awet akikata utepe kuzindua rassmi ugawaji wa Pipikipi 200 kwa Wachungaji wilayani Hanang' mkoani Manyara.
Sehemu ya Pikipiki 200 zilizogawiwa kwa Wachungaji wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God (PAG), wilayani Hanang' mkoani Manyara kwa ajili ya kazi ya kuhubiri Injili.
Mkurugenzi wa Kampuni ya MCB Investiment Mchungaji Alex Mapanga katikati akimuonyesha namba za moja ya Pikipiki zilizogawiwa kwa Wachungaji wilayani Hanang' mkoani Manyara Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentecostal Assembilies of God (PAG), Daniel Awet. 
Mkurugenzi wa Kampuni ya MCB Investiment Mchungaji Alex Mapanga akifafanua jambo kuhusu Pikipiki hizo mbele ya viongozi wa dini wakati wa zoezi la ugawaji Pikipiki hizo kwa Wachungaji. 
Mkuu wa Polisi wilaya ya Hanang' mkoani Manyara (OCD), Sweetbert Tryphone akimshukuru Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God (PAG), Daniel Awet mara baada ya kumkabidhi Pikipiki moja kwa ajili ya jeshi la polisi. 

No comments:

Post a Comment