Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amefanya mabadiliko ya makamanda wa polisi kwa baadhi ya mikoa.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Julai 3, 2018  iliyosainiwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa, inasema mabadiliko hayo yanalenga kuongeza juhudi za kuzuia ajali zilizotokea mara kwa mara katika baadhi ya mikoa.

Katika mabadiliko hayo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Deusdedit Nsimeki aliyekuwa makao makuu ya upelelezi Dar es Salaam anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Simiyu.

Aliyekuwa RPC Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei anakwenda kuwa RPC Mkoa wa Mbeya.

Katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Kaimu RPC Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi, Mussa Taibu amehamishiwa makao makuu ya polisi Dar es Salaam.

Aliyekuwa RPC Mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Wilbroad Mutafungwa anakwenda kuwa RPC Mkoa wa Morogoro, nafasi yake ikichukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Emmanuel Nley kutoka makao makuu ya polisi Dar es Salaam.

Wengine waliohusika na mabadiliko hayo ni aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi wa Polisi, Stanley Kulyamo anayekwenda kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Tazara.

IGP Sirro amewataka makamanda wa polisi wa mikoa nchini, kuendelea kuwajibika ipasavyo katika kuhakikisha ajali hazitokei katika maeneo yao na kuwachukulia hatua kali madereva watakaosababisha ajali kwa uzembe.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: