Wednesday, 4 July 2018

Abiria wakesha polisi kisa ubovu wa mabasi


ZAIDI ya abiria 70 kati ya 120 waliokuwa wakisafiri na mabasi mawili ya kampuni ya King Msukuma,  yaliyokuwa yakifanya safari kati ya Mwanza na Bukoba na lingine Bukoba na Mwanza, wamekesha kituo cha polisi kutokana na ubovu wa mabasi.

Abiria hao walikesha baada ya mabasi yao kukamatwa kutokana na ubovu uliokithiri huku baadhi ya vipuri vikiwa vimefungwa kwa kamba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Latson Mponjoli, alisema jana kuwa magari hayo yalikamatwa juzi jioni ikiwa sehemu ya operesheni ya ukaguzi wa mabasi ya abiria iliyodumu kwa wiki tatu sasa.

Kwa mujibu wa kamanda Mponjoli, mabasi hayo ni kati ya 59 yaliyokaguliwa katika operesheni hiyo na 47 kati yake  yalikutwa na kasoro kidogo yakaruhusiwa kuendelea na safari huku mengine manane yakilipa faini na manne yakizuiwa kuendelea na safari.

Mponjoli aliyataja mabasi yaliyokamatwa na kuzuiwa kuendelea na safari kuwa ni yenye namba za usajili T746 BMP aina ya Scania lililokuwa likiendeshwa na Kini Daudi na lingine lenye namba za usajili T950 CGU aina ya Zomtong lililokuwa likiedeshwa na Omary Aloys.

Alisema mabasi hayo ni mali ya kampuni ya King Msukuma na yanamilikiwa na Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku maarufu kama Musukuma na kwamba madereva hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.

Kamanda Mpojoli amesema jeshi la polisi lilizuia mabasi hayo kuendelea na safari kwa sababu za kiusalama kwa maisha ya abiria kutokana na ukubwa wa kasoro zilizogunduliwa wakati wa ukaguzi.

Moja ya kasoro hizo, kwa mujibu wa kamanda huyo ni moja ya mabasi kufungwa kamba kwenye ‘propeller shafti’ huku mabasi yote yakiwa na ubovu pia wa ‘shock absorber’ na ubovu katika ‘steering box’.

Kutokana na kukwama huko kwa abiria, Mponjoli alisema jeshi lilitafuta usafiri mbadala wale waliokuwa wakienda Bukoba na wakati huo huo polisi wakiandaa utaratibu wa kuwafikisha madereva wa mabasi mabovu mahakamani.

Baadhi ya abiria walisema waliingiwa na hofu kwa usalama wao baada ya mabasi kukaguliwa kubainika kuwa vipuri vimefungwa kwa kamba.

Mabasi hayo yamekamatwa ikiwa wiki chache baada ya basi lenye namba za usajili T204 CGW pia mali ya kampuni ya King Msukuma kupata ajali Juni 18, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu watano na kujeruhi wengine 36.

Basi hilo lililosababisha ajali na vifo hivyo kikiwamo cha mtembea kwa miguu katika mtaa wa Magogo, Halmashauri ya Mji wa Geita likiwa safarini kutoka Mwanza kwenda Bukoba.

No comments:

Post a Comment