Monday, 4 June 2018

Yanga waidhalilisha Tanzania nchini Kenya


Kichapo cha mabao 3-1 ilichopata Yanga jioni huu kutoka kwa Kakamega Homeboys ya Kenya, kimeilazimisha timu hiyo kurejea nchini baada ya kuondolewa kwenye michuano ya SportsPesa Super Cup inayoendelea nchini Kenya.

Yanga imefungwa mabao hayo katika mchezo wa kwanza wa mashindano hayo ambayo yameanzia hatua ya robo fainali hivyo timu inayofungwa ni lazima iage mashindano na kurudi nyumbani kama ambavyo imekuwa kwa Yanga.

Mabingwa hao wa zamani wa Tanzania, waliruhusu mabao 2 - 1 katika kipindi cha kwanza, kabla ya kukubali bao la tatu kipindi cha pili na kuwanyima nafasi ya kwenda kucheza na Everton huko England ambapo nafasi hiyo anaipata bingwa wa michuano hiyo.

Yanga sasa imeshindwa kupata ushindi kwenye mechi 11 kati ya 12 ilizocheza hivi karibuni katika mashindano yote ikiwemo Ligi kuu iliyomalizika Mei 28, Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na michuano hii.

Kakamega Homeboys ni timu inayoshiriki ligi kuu ya soka ya Kenya na inashika nafasi ya 9 kwenye msimamo ikiwa imecheza mechi 17, ikishinda 7, sare 3 na kupoteza 7 na ina alama 24.

No comments:

Post a Comment