WILAYA ya Karatu imegawa maeneo kwa wafanyabiashara wadogo wakiwamo  mamalishe na wamachinga ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara.

Migogoro mingi imekuwa ikisababishwa na makundi hayo kufanya shughuli zao maeneo yasiyo rasmi na kujikuta wakifukuzwa .

Mkuu wa Wilaya hiyo, Theresia Mahongo, alisema kuwa Wilaya hiyo imeamua kuwatengea maeneo katika eneo la Mnadani ili kumaliza mgogoro uliokuwapo tangu mwaka 2000 baada ya wafanyabiashara hao waliokuwa wakifanya biashara pembezoni mwa barabara kuondolewa ili kupisha ujenzi wa barabara ya Karatu /geti la Ngorongoro.

Maqhongo alisema kuwa wamewagawia maeneo hayo ambayo wanaweza kujenga vibanda na kuweka mkataba na halmashauri juu ya ulipaji wa kodi ili wafanye kazi zao bila kubughudhiwa na kujipatia kipato cha kila siku

Alisema jumla ya wafanyabiashara 34 watagawiwa maeneo katika eneo la Mnadani ambapo wanatarajia kulitumia eneo hilo katika biashara ndogo ndogo kwani wanatarajia kuwa eneo hilo litaendelezwa na kuwa na mzunguko mkubwa wa biashara.

Mkurugenzi Mtendaji  wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Waziri Mourice, alisema kuwa wataandaa mikataba ambayo itawasilisha maslahi ya pande zote mbili, na kuongeza kuwa mpango huo unalenga kuwawezesha wananchi wanyonge kupata maeneo ya kufanya shughuli zao kama ilivyo serikali ya awamu ya tano ambayo imejipambanua kuwahudumia wananchi wanyonge.

“Mpaka tarehe 15  mwezi huu tutakuwa tumeandaa mikataba baina ya halmashauri na wafanyabiashara ili waweze kuwa huru kujenga vibanda vyao na kuanza  ujenzi na kufanya shughuli zao,” alisema Mkurugenzi huyo.

Kwa Upande wao wafanyabiashara hao, Evelina  Hando na  Fausta Saria waliishukuru serikali kwa kusikiliza kilio chao cha muda mrefu cha kuwapatia maeneo ya kufanya shughuli zao kwani kwa muda mrefu walikuwa wakiteseka na kukosa maeneo rasmi.

Evelina alisema  wamekua wakiteseka tangu mwaka 2000 wamehamishwa mara kwa mara na kuibuka migogoro kati yao na wamiliki wa maeneo walipokuwa wanafanyia biashara, lakini kwa sasa wanaishukuru serikali   kwa kuwapatia maeneo hayo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: