Monday, 4 June 2018

Tundu Lissu Kufanyiwa Upasuaji Mwingine Leo

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu leo Juni 4, 2018 atafanyiwa upasuaji wa 21 wa kuunga goti la mguu wake wa kulia huku akiwataka Watanzania kumuombea.

Upasuaji huo ni mwendelezo wa upasuaji ambao amekuwa akifanyiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikokuwa amelazwa baada ya kushambuliwa kwa risasi akiwa katika makazi yake mjini Dodoma Septemba 7, 2017.

Alipatiwa huduma za awali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Lissu ameeleza hayo leo Jumapili Juni 3, 2018 kupitia taarifa aliyoitoa katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram, akiambatanisha na picha yake akiwa amelala wodini kando ya mkewe, Alicia.

“Hello  wapendwa wangu. Ninaamini wengi wenu, kama sio wote, mnafahamu kwamba Jumatatu Juni 4 nitafanyiwa operesheni ya mwisho kwenye mguu wa kulia,” amesema.

“Ni operesheni kubwa inayotazamiwa kuchukua takriban saa nane kwa taarifa nilizopewa tangu mwanzoni mwa wiki hii. Hivyo madaktari wangu wametumia muda mrefu kidogo kuniandaa kwa ajili ya Jumatatu.”

Ameongeza, “Napenda niwajulishe kwamba ninajisikia vizuri kiafya na baada ya kuwa kitandani tangu  Aprili 11 (2018) nilipofanyiwa operesheni ya pili, sasa niko tayari kwa ajili ya hii ya mwisho. Madaktari wangu wako vizuri. Nina imani watafanya kazi nzuri ya kitabibu.”

Lissu alishawashukuru wote waliomsaidia tangu aliposhambuliwa kwa risasi hadi sasa na kuwataka wazidi kumuombea.

“Bado safari ni ndefu lakini ninaweza kusema nimeanza kuona mwanga katika hili tanuru refu. Nimesema mara nyingi kwamba ninaona fahari na faraja kwamba Watanzania wenzangu na wasio Watanzania wamenitibu na wanaendelea kunitibu. Najua mtaniponya kwa nguvu za Mola wetu na kwa upendo na ukarimu wenu. Nawaombeni msichoke. Nawashukuruni sana,” amesema.

No comments:

Post a Comment