Rais wa Marekani, Donald Trump alisema alhamis kwamba atamualika kiongozi wa Korea kaskazini, Kim Jong Un kuja Marekani kama mkutano ujao wa kihistoria na kiongozi huyo utakuwa na mafanikio. Kwa upande mwingine, alisema yuko tayari kujiondoa kwenye mkutano ikiwa mambo hayatakua sawa.

Rais Trump alikutana kwa saa mbili na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe huko White House siku ya alhamis chini ya wiki moja kabla ya mkutano wake wa kilele na Kim Jong Un huko Singapore.

Mkutano huo na Korea kaskazini pia masuala ya biashara yalizingatiwa zaidi wakati wa majadiliano yao. Abe alitaka uhakikisho kutoka Marekani kwamba hatua zitafanywa kudhibiti mipango ya nyuklia na makombora ya masafa marefu ya Korea kaskazini. Pia alitaka Rais Trump kuzungumza na Kim suala la raia wa Japan waliotekwa nyara na Korea kaskazini wakati wa miaka ya 1970 na 1980.

Kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, baada ya mazungumzo yao, Trump alimuahidi Abe kwamba atalizungumzia suala hilo wakati wa mkutano wake na Kim.

Rais Trump pia alisema yupo wazi kutia saini makubaliano ya Juni 12 na Korea kaskazini kumaliza rasmi vita vya Korea, lakini alitahadharisha kwamba hiyo ni hatua ya kwanza tu. Trump pia aliwaambia waandishi wa habari kwamba angependa kuona hatimaye uhusiano kati ya Marekani na Korea kaskazini unarudishwa tena.

Trump alipongeza ushirikiano kati ya Japan na Korea kusini katika miezi ya hivi karibun uliowezesha mkutano huo na vile vile kumshukuru Rais wa China, Xi Jinping kwa kusaidia katika utaratibu huo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: