Thursday, 7 June 2018

Tarehe kuanza ‘flyover’ Tazara yatajwa


WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, amesema jaribio la kwanza la kupitisha magari katika barabara za juu ‘flyover’ iliyoko makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara, Dar es Salaam, litafanyika Agosti, mwaka huu.

Amesema daraja hilo hadi sasa limeshakamilika kwa asilimia 88.82 na litazinduliwa rasmi Septemba na Rais John Magufuli.

Prof. Mbarawa aliyasema hayo jana alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo linalojengwa na Kampuni ya Sumito Mitsui Construction Co Ltd kutoka Japan kwa gharama ya Sh. bilioni 95.

“Gari la kwanza litapita kwenye daraja hili mwezi wa nane na nitasimamia mimi mwenyewe kabla ya Rais Magufuli hajaja kuzindua. Hatuwezi  kumleta Rais kabla ya kulifanyika majaribio,” alisema Prof. Mbarawa.

Waziri alisema kwa sasa ujenzi wa daraja hilo uko katika hatua za mwisho, kilichobakia ni ujenzi wa maeneo ya kuingilia ambayo yako eneo la mwisho.

 Alisema tangu ujenzi huo uanze hadi jana hakuna ajali yoyote iliyotokea na kwamba wajenzi wanazingatia sheria na taratibu za ujenzi.

Kadhalika, Prof. Mbarawa alisema mbali na ujenzi wa ‘flyover’ hiyo, pia kutajengwa  nyingine kama hiyo katika maeneo ya Kurasini, Chang’ombe, Mwenge na Morocco, lengo likiwa kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.

Naye Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshinda, alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Japan utazidi kuongezeka na kwamba tangu ujenzi wa daraja hilo unaanza askari wa usalama barabarani wamefanya kazi kubwa kufanikisha.

Rais John Magufuli wakati akiweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa ‘flyover’ hiyo alisema kuwa gharama za mradi huo ni Sh. bilioni 100 na kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 93.44 zitatolewa na serikali ya Japan kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa (JICA), huku Sh.bilioni 8.3 zikitolewa na serikali ya Tanzania.

Pia alisema barabara ya juu itakayojengwa itakuwa na njia nne na urefu wa mita 300 kutoka maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) itakayopunguza kero na msongamano wa magari yanayoenda na yatokayo JNIA na bandari ya Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment