Tuesday, 5 June 2018

Spika Ndugai ahoji muonekano wa suti za Sugu


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ameshindwa kujizuia na kuhoji muonekano wa suti za Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi kwa kutaka kufahamu kwa nini pamoja na kuvaa suti nzuri lakini bado zinaonekana na namba ambazo hazieleweki.

Spika Ndugai amehoji hayo wakati Mbunge huyo akitoa mchango wake katika bajeti ya wizara ya fedha na mipango kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Wakati akihoji swali lake kwa Mbunge huyo, Ndugai aliuliza, "Kabla sijakuongezea dakika moja waheshimiwa wengi wameniandikia kwamba umevaa suti nzuri sana lakini umeweka lebo za ajabu hiyo 219 ni kitu gani?

Akijibu swali hilo Sugu amesema "Hii ni namba yangu ya mfungwa jela, ambayo nitaendelea kuvaa kadiri ambavyo nitajisikia. Kuhusu Suti Mh. Spika wewe unanijua ni kawaida yangu kupiga suti kali".

Hata hivyo baada ya jibu hilo Spika Ndugai amemuahidi Mbunge huyo kufuatilia zaidi katika kanuni zake kama inaruhusiwa kuvaa namba za magereza ndani ya jengo la Bunge.

Hivi karibuni Mbunge huyo kutoka Mbeya mjini amekuwa akionekana akivaa nguo zenye namba 219 mbele ambapo huwa akifafanua kwamba ilikuwa namba yake siku alipoingia magereza ya Ruanda baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi 5 kwa kosa la kutoa lugha chafu dhidi ya Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment