Serikali imesema haitavumilia vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika baadhi ya shule hapa nchini na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako mkoani Dodoma wakati akikabidhi tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa katika masomo yao ya kuhitimu darasa la saba, Kidato Cha Nne na kidato Cha Sita kwa shule za serikali na zisizokuwa za serikali.

Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi nchini kote kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu pamoja na kuishi kwa kufuata maadili ya kitanzania na siyo kuiga maadili ya watu wa nje.

“Wakuu wa shule nchini kote nawaagiza kuhakikisha mnasimamia kwa weledi malezi ya wanafunzi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha walimu mnakemea vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika shule hapa nchini. Suala hili nasema si la kufumbia macho na wale wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa,” amesema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amewaeleza wanafunzi hao kuwa suala la kupata ushindi ni rahisi lakini kudumu katika ushindi si Kazi nyepesi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge amewapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao kitaifa ambapo amesema Silaha pekee ya ujenzi wa Taifa na rasilimali za Taifa ni Elimu, ambapo pia amewataka wanafunzi kudumisha nidhamu  na maadili.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Uingereza katika maadhimisho hayo ya wiki ya Elimu Gertrude Mapunda  amesema serikali ya Uingereza itaendelea kuisaidia  Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya Elimu.

Imetolewa na:
kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
8/6/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: