Na Kadama Malunde
Watu wanne wanaodaiwa kuwa ni majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi eneo la makaburi  ya Kitwana kata ya Busoka tarafa ya Kahama Mjini wilayani Kahama wakati wakijaribu kuwatoroka askari waliokuwa kwenye msako mkali wa kuwatafuta majambazi wanaojihusisha na matukio ya uhalifu katika wilaya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makaburi ya Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama jana Jumatatu Juni 4,2018,Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule alisema tukio hilo limetokea Juni 3,2018 majira ya saa sita na dakika 40 mchana.

Amewataja waliouawa kuwa ni Minani Deo (33) mkazi wa Mabanda Burundi ambaye pia ni muagizaji wa silaha haramu kutoka nchi jirani na Masalamali Paulo (34) mkazi wa Geita ambaye aliachiwa kwa msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia Dkt. John Pombe Magufuli katika gereza la Butimba mkoani Mwanza mwezi Aprili 2018.

Wengine waliouawa ni Hussein Issa Jumanne maarufu kwa jina la Shehe (30) mkazi wa Nyasubi Kahama,Maduhuli Cheyo Maselegu (42) mkazi wa Kigoma Ujiji.

Akielezea zaidi kuhusu tukio hilo,Kamanda Haule alisema siku ya tukio watu hao walijeruhiwa kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za miili yao na kufariki dunia wakiwa wanapelekwa hospitali ya Mji wa Kahama.

“Walikuwa wanaelekea kuwaonyesha askari polisi bastola na bomu moja la kutupwa kwa mkono ‘Hand Grenade) pamoja na washirika wenzao wa ujambazi,wakiwa tayari wameonesha bastola na bomu hilo lililokuwa limechimbiwa chini ya ardhi ndipo walipotaka kuwakimbia askari na askari wakawafyatulia risasi”,alifafanua Kamanda Haule.

“Chanzo cha tukio hilo ni kutaka kuwatoroka askari waliokuwa kwenye msako mkali wa kuwatafuta majambazi wanaojihusisha na matukio ya uhalifu hasa katika wilaya ya Kahama kwa kipindi cha mwezi Machi hadi Mei 2018”,aliongeza.

Aidha alisema takwimu zinaonesha majambazi hao walikimbilia mkoani Tabora na mara baada ya askari kufika mkoani Tabora wakapata taarifa kuwa majambazi hao wamekimbilia mkoani Kigoma na polisi kufanikiwa kumkamata Masalamali Paulo eneo la soko la Mwanga mkoani Kigoma.

“Baada ya kumkamata na kumhoji aliwataja washirika wenzake watatu wa ujambazi ambao walikimbilia Katumba mkoani Katavi na kufanikiwa kuwakamata wakiwa na silaha ya kivita aina ya AK47 yenye namba UA-2651-1997 iliyokuwa na risasi 30 ndani ya magazine moja ambayo ilipatikana karibu na uwanja wa ndege mkoani Katavi”,alieleza.

Aliongeza kuwa silaha hiyo pia ilikuwa imehifadhiwa pamoja na bastola moja aina ya Browning yenye namba 17569465 ikiwa na risasi 15 ndani ya magazine yake ndani ya shimo.

Alisema katika mahojiano na majambazi hao walikiri kufanya matukio ya uhalifu katika wilaya ya Kahama na mikoa ya Tabora,Geita,Morogoro,Kigoma na Katavi na kwamba miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya Mji wa Kahama.

Wakati huo huo,Kamanda Haule alisema mnamo tarehe 28.5.2018 majira ya saa moja na nusu usiku katika mtaa na kata ya Mhungula wilayani Kahama ikipatikana silaha moja aina ya shortgun yenye namba B-15939 iliyokuwa imekatwa kitako na mtutu ikiwa imehifadhiwa kwenye mfuko wa sulphate ndani ya nyumba ya Malale Kalikisu Malale aliyekuwa anatafutwa na polisi kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Alisema mtuhumiwa alikimbia kabla ya kukamatwa na juhudi za kumtafuta na kumkamata zinaendelea.

Kamanda Haule amewataka wahalifu wote kujisalimisha pamoja na silaha zao ndani ya mkoa au nje ya mkoa na wasipofanya hivyo wataendelea kuwafuatilia sehemu yoyote waliyojificha iwe chini ya ardhi,angani au ziwani ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Mheshimiwa rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Magufuli kwa mapenzi yake na wananchi wake,kwa huruma yake aliamua kuwaachia huru wahalifu waliokuwa wamefungwa gerezani akiwemo huyu Masalamali Paulo warudi uraiani,wajirekebishe na washiriki kwenye shughuli za uchumi,sasa baadhi ya hao wahalifu wanauchukulia huu msamaha katika njia ambazo siyo sahihi,hivyo wote walioachiwa kwa msamaha wa rais waendane na maadili mema katika jamii”,alieleza.

“Ndugu wananchi naomba turejee kauli ambayo inatolewa mara kwa mara na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Nyakoro Sirro kuwa uhalifu haulipi, uhalifu hauna nafasi nami pia naungana na kauli ya afande IGP kurudia maneno hayo hayo kuwa kwa sasa uhalifu mkoani Shinyanga hauna nafasi,tunataka wananchi wafurahie matunda ya uhuru,matunda ya uhuru ni amani na utulivu",

"Wananchi wafanye shughuli zao za kiuchumi bila ya kuwa na hofu yoyote ile ya matishio ya kiusalama ili kusudio la kuleta maendeleo katika jamii litimie,natoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi mapema”,alisema.
  
Credit :Malunde
Share To:

msumbanews

Post A Comment: