Mikataba ya Utendaji, kigezo ni taasisi husika kuwa na bodi hai na kuwa na bajeti iliyoidhinishwa. Matokeo ya tathmini yanaonesha wastani wa taasisi kufanya vizuri kwa asilimia 70.

36.     Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea kufanya uchambuzi wa taasisi na mashirika ya umma ambayo majukumu yao kwa namna moja au nyingine yanafanana kwa lengo la kuunganisha taasisi hizo ili kuongezea tija na kupunguza gharama za uendeshaji.

37.     Mheshimiwa Spika, shughuli zingine zilizotekelezwa katika kusimamia Mashirika na Taasisi za Umma nikama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 37 hadi ukurasa wa 39.

2.1.14        Mafao ya Wastaafu na Mirathi

38.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 1,008.61 kwa ajili ya kulipia michango ya mwajiri kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.  Hadi kufikia Aprili, 2018 kiasi cha shilingi bilioni 716.19 sawa na asilimia 71kilitumika kulipa michango ya mwajiri kwa watumishi wa umma. Aidha, nitumie fursa hii kuiagiza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iandikishe wanachama wake, kuwapa vitambulisho vya uanachama na kutunza vizuri na kwa usahihi taarifa za uchangiaji kwa kipindi chote cha utumishi wa wanachama ili kuwaondolea usumbufu siku za kustaafu kwao kama ilivyoelekezwa na Miongozo ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Vile vile, ninawakumbusha watumishi wa Umma wawe na tabia ya kukagua taarifa za madaraja ya mishahara, makato ya lazima na yale yasiyo ya lazima kutoka kwenye mishahara yao na kutoa taarifa kwa wakati kwa mamlaka husika ili kama kuna makato hayako sawasawa mamlaka husika zichukue hatua za kurekebisha mapema na kuisaidia Serikali kuepuka tozo zinazoweza kutozwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Taasisi nyingine za fedha.

39.     Mheshimiwa Spika, shughuli zingine zilizotekelezwa katika kusimamia Mafao ya Wastaafu na Mirathi nikama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 39 hadi ukurasa wa 41.

2.1.15        Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi

40.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi kimeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu kwa kufanya yafuatayo: Kupokea na kuchambua taarifa 254 za miamala shuku inayohusu fedha haramu na ufadhili wa ugaidi na kuwasilisha taarifa za kiintelijensia 32 kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria kwa ajili ya uchunguzi. Aidha, katika kujenga uwezo wa watumishi, Maafisa wa Kitengo walipata mafunzo ya namna bora ya uchambuzi na upembuzi wa taarifa za miamala shuku katika Kituo cha Kudhibiti Fedha Haramu (Financial Intelligence Centre – FIC) cha Afrika ya Kusini na Maafisa wanne (4) walihudhuria mafunzo yaFinancial Action Task Force (FATF)standards yaliyofanyika nchini Korea Kusini ambayo ni muhimu katika nyanja ya udhibiti wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.

41.     Mheshimiwa Spika, shughuli zingine zilizotekelezwa katika kusimamia utekelezaji wa Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi nikama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 41 hadi ukurasa wa 43.

2.1.16        Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP)

42.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara imeendelea kuratibu na kuchambua miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi na kuishauri Serikali juu ya utekelezaji wa miradi hiyo. Aidha, kulingana na Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi Sura 103; uchambuzi wa miradi ya Ubia hupitia hatua tatu zifuatazo; (i) Mamlaka za utekelezaji kuwasilisha andiko la awali la mradi kwa ajili ya uchambuzi (ii) Mamlaka kuandaa taarifa ya awali ya upembuzi yakinifu (iii) Mamlaka ya utelekezaji wa miradi ikishirikiana na Mshauri Elekezi kuandaa na kuwasilisha Taarifa ya Upembuzi Yakinifu. Wizara hufanya uchambuzi wa taarifa hizo kwa kuangalia, pamoja na mambo mengine maeneo makuu matatu: (a) Uhamishaji wa mianya hasi ya mradi kwenda kwa sekta binafsi; (b) Uwezo wa Serikali kugharimia mradi; na (c) Manufaa ya mradi kwa Serikali  na wananchi kwa ujumla. Endapo mradi unakidhi vigezo utaidhinishwa na Kamati ya Wataalam wa PPP kwa ajili ya kuendelea na hatua ya kumpata mbia.

43.     Mheshimiwa Spika, Wizara imefikia hatua mbalimbali za uchambuzi wamiradi itakayotekelezwa kwa utaratibu wa PPP. Upembuzi Yakinifu wa Mradi wa Uzalishaji wa Madawa muhimu na Vifaa Tiba wa Bohari Kuu ya Madawa (MSD) umekamilishwa na kuwasilishwa kwenye Kitengo cha Ubia kwa ajili ya hatua za uidhinishaji; Mradi wa Kujenga na Kuendesha Vyuo 10 vya VETA kwa Utaratibu wa PPP katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Manyara, Tabora na Shinyanga.Wizara  imefanya uchambuzi wa Taarifa ya Upembuzi Yakinifu na kuwasilisha kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mapendekezo  yanayotakiwa kuzingatiwa ili mradi uwe na tija kwa Taifa; Mradi wa Barabara ya Tozo kutoka Dar Es Salaam hadi Chalinze, taarifa ya upembuzi yakinifu wa mradi imefanyiwa uchambuzi ambapo Wizara imetoa idhini yenye masharti (Conditional Approval) ya kutekeleza  kabla ya kuendelea na hatua ya kumpata mbia; Mradi wa Uendeshaji wa Huduma ya Usafiri jijini Dar es Salaam Awamu ya kwanza, zabuni kwa ajili ya ununuzi wa mtoa huduma wa kudumu, mkusanyaji mapato na mwendesha mfuko zilitangazwa na wazabuni wamepatikana; na Wizara imekamilisha uchambuzi wa andiko la awali la mradi wa Mradi wa Mwambani Port lililowasilishwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania, hatua inayoendelea ni maandalizi ya Upembuzi Yakinifu.

44.     Mheshimiwa Spika, shughuli zingine zilizotekelezwa katika kusimamia utekelezaji wa PPP ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 44 hadi ukurasa wa 46.

2.2            USIMAMIZI NA URATIBU WA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA CHINI YA WIZARA

45.     Mheshimiwa Spikakama nilivyoeleza hapo awali, Wizara yangu inaratibu na kusimamia mashirika na taasisi za umma 36 zilizo chini yake. Utekelezaji wa majukumu ya taasisi na mashirika haya kwa mwaka 2017/18 ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 47 hadi ukurasa wa 78.  Aidha, utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Wizara kwa mwaka 2017/18 ni kama unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanziaukurasa wa 79 - 81.

2.3          CHANGAMOTO NA HATUA ZILIZOCHUKULIWA

2.3.1           CHANGAMOTO

46.        Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango, changamoto zilizojitokeza ni pamoja na:
                                i.             Ukwepaji wa kodi;
                               ii.             Kuchelewa kupatikana kwa misaada na mikopo ya masharti nafuu pamoja na mikopo ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo;
                             iii.             Uelewa mdogo wa wananchi juu ya dhana ya utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi ambayo ni pana na inabadilika kwa kasi;
                             iv.             Baadhi ya wawekezaji kutelekeza mali walizouziwa na Serikali wakati wa zoezi la Ubinafsishaji; na
                               v.             Uelewa mdogo wa dhana ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.

2.3.2           HATUA ZA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO

47.        Mheshimiwa Spikakatika kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa bajeti, Wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo:
                                i.             Kutekeleza mkakati wa ulipaji kodi kwa hiari na kuendelea kuboresha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kwa kujenga mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato;
                               ii.             Kuendelea kuelimisha wadau mbalimbali kupitia makongamano, mikutano na warsha kuhusu dhana ya utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi;
                             iii.             Kuendeleza mazungumzo na Washirika wa Maendeleo kuhusu njia mpya za kutoa na kupokea misaada na mikopo (New Financing Instruments);
                             iv.             Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeongeza nguvu   katika kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa wawekezaji wote ili kuhakikisha wanaendesha viwanda na mali walizouziwa kwa kuzingatia Masharti ya Mikataba ya Mauzo; na
                               v.             Kuendelea kutoa mafunzo kuhusu ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa watumishi wa umma na sekta binafsi.

3.0       MALENGO YA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2018/19

48.        Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2018/19 umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016 /17- 2020/21), Sheria ya Bajeti Na.11 ya Mwaka 2015, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi – CCM (2015 – 2020), Hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati wa Uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na masuala mtambuka kama vile Jinsia, watu wenye ulemavu, Mazingira, UKIMWI, makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi na masuala ya lishe kwa jamii pamoja na maelekezo na ahadi zilizotolewa Kitaifa.

3.1       MPANGO WA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA

3.1.1           Kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Uchumi Jumla

49.        Mheshimiwa Spika, shabaha za uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:-
(i)           Pato la Taifa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka 2018 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 7.1 mwaka 2017;
(ii)          Mfumuko wa bei kuendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja;
(iii)        Mapato ya ndani kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 15.3 mwaka 2017/18 na asilimia 15.6 mwaka 2016/17;
(iv)        Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.6 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 13.0 mwaka 2017/18 na asilimia 13.3 mwaka 2016/17; na
(v)          Nakisi ya bajeti kufikia asilimia 3.2 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 2.1 mwaka 2017/18 na asilimia 1.5 mwaka 2016/17.

3.1.2           Uratibu wa Mipango ya Maendeleo ya Taifa

50.        Mheshimiwa Spika, kutokana na kuunganishwa kwa iliyokuwa Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha, imebidi kuupitia muundo wa Wizara ili uweze kuyaingiza mabadiliko haya ili kutoathiri utekelezaji wa majukumu pamoja na maslahi ya watumishi kwa ujumla. Muundo wa Wizara uko katika hatua za mwisho za kuidhinishwa na Mamlaka husika, ambapo imependekezwa iundwe Divisheni ya Mipango ya Maendeleo ya Taifa itakayoongozwa na Kamishna na kuwa na kifungu chake.

51.        Mheshimiwa Spika, hivyo katika mwaka 2018/19, shughuli za kipaumbele zitakazotekelezwa katika uratibu wa mipango ya maendeleo ya Taifa ni pamoja na: Kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20; Kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/19; Kufanya tathmini ya muda wa kati katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano; Kukamilisha uundwaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi wa miradi ya kitaifa ya Maendeleo; na Kufuatilia matumizi ya Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Management - Operational Manual - PIM – OM).

3.1.3           Uratibu wa Mikakati ya Kupunguza Umaskini

52.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara itaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa juhudi za kupunguza umaskini ikiwemo kusimamia utekelezaji wa Mfumo wa  Ufuatiliaji wa Jitihada za Kuondoa Umaskini nchini (Poverty Monitoring System - PMS); kufuatilia utekelezaji wa malengo yaliyoainishwa katika Mipango ya kitaifa na kisekta na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 2030 na programu zinazolenga kuondoa umaskini katika maeneo ya vijijini na mijini; kufanya uchambuzi wa kina juu ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya (HBS-2017/18); kutoa mafunzo kwa Maafisa Mipango na Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhusu jitihada za kupambana na umaskini na kutunza mazingira ili kuweza kujumuisha katika mipango na bajeti zao.

53.        Mheshimiwa Spika, Mipango mingine katika uratibu wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini iko katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 87 hadi ukurasa wa 89.

3.1.4           Usimamizi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali

(a)        Mapato ya Ndani

54.        Mheshimiwa Spika, katika kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka 2018/19, Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo: kusimamia sera za fedha na za kibajeti zinazolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara; kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari kwa kuimarisha Mkakati Shirikishi wa Mawasiliano na Walipa kodi na kuboresha utaratibu wa utozaji kodi; kujenga uwezo  wa watumishi ili kukabiliana na tatizo la uhamishaji faida (Transfer Pricing) unaofanywa na kampuni zenye mitandao ya kimataifa kwa lengo la kukwepa au kupunguza kodi; kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa ulipaji kodi kupitia Mfumo wa Vitalu vya Walipakodi; kusimamia zoezi la uunganishaji wa Wizara, Idara, Wakala, taasisi na mashirika ya umma kwenye Mfumo wa Serikali wa  Kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato (GePG)   ili  kuboresha ukusanyaji  na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali; na kuongeza kasi ya uthaminishaji wa majengo ili kuongeza mapato yatokanayo na kodi ya majengo.

55.        Mheshimiwa Spika, mikakati mingine iliyopangwa iko katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 89 hadi ukurasa wa 90. 

(b)       Misaada na Mikopo

56.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara itaendelea na uratibu wa upatikanaji wa fedha za misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kwa ajili ya kugharamia programu na miradi ya maendeleo mbalimbali nchini. Washirika wa Maendeleo wameahidi kuchangia Bajeti ya Serikali kiasi cha shilingi bilioni 2,676.64. Kati ya fedha hizo,  shilingi bilioni 545.76 ni kwa ajili ya Misaada na Mikopo nafuu ya Kibajeti (GBS), shilingi bilioni 125.86 kwa ajili ya Mifuko ya Pamoja ya Kisekta na shilingi bilioni 2,005.02  kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

57.        Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na: kukamilisha Mpango Kazi wa kutekeleza Mwongozo mpya wa ushirikiano (Development Cooperation Framework- DCF); nakukagua miradi inayofadhiliwa na Washirika wa Maendeleo.

3.1.5           Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali

58.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo: kuendelea kuboresha Mfumo mpya wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti ya Serikali (CBMS) ili kurahisisha utoaji  wa mgao wa fedha za matumizi kila mwezi na kuendesha mafunzo ya mfumo huokufanya marekebisho, kuchapisha na kusambaza nakala 2,200 Vitabu vya Makadirio ya Matumizi ya Serikali ya mwaka 2018/19 kama yalivyopitishwa na Bunge, kuchapisha na kusambaza: Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2019/20, Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali za kila Robo Mwaka, Vitabu vya Makadirio ya Matumizi ya Serikali ya mwaka 2019/20 na kuviwasilisha Bungeni na kuvisambaza kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa  kwa Wadau wengine.

59.        Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizopangwa kufanyika ziko katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 92 hadi ukurasa wa 93.

3.1.6           Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Serikali

60.        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018/19, Wizara itaendelea kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kufanya ufuatiliaji wa uzingatiaji wa miongozo mbalimbali ya ukaguzi wa ndani iliyotolewa na Wizara na kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa ndani katika maeneo ya ukaguzi wa miradi, ukaguzi wa kiufundi, usimamizi wa vihatarishi, mfumo wa usimamizi wa kazi za ukaguzi na mfumo wa kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

61.        Mheshimiwa Spika, mipango mingine ambayo Wizara inatarajia kutekeleza katika usimamizi wa udhibiti wa fedha za umma iko katika hotuba yangu ukurasa wa 94 hadi ukurasa wa 95.

3.1.7           Usimamizi wa Malipo

62.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepanga kusimamia mfumo wa udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Akaunti Jumuifu  (Treasury Single Account) kwa lengo la kuboresha mfumo wa matumizi ya Umma ili kuiongezea Serikali uwezo wa  kugharamia shughuli zake kwa wakati. Aidha, Wizara itaendelea na usimikaji na usimamizi wa mifumo ya malipo ya kieletroniki (EFT na TISS) ili kuondoa ucheleweshaji wa malipo kwa wadau mbalimbali wakiwemo wastaafu, watoa huduma kwa Serikali pamoja na watumishi wa Umma. Vile vile, Wizara itaendelea na uunganishaji wa mfumo wa Malipo (Epicor) kwenye Balozi saba (7) ili kudhibiti matumizi nje ya bajeti.

3.1.8           Deni la Serikali

63.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Serikali itahakikisha kuwa Deni la Serikali linaendelea kuwa himilivu na kutokuwa mzigo kwa uchumi wetu na kuendelea kuwa fursa na kichocheo cha maendeleo kwa nchi yetu. Aidha, Serikali itaendelea kukopa kwa uangalifu kwa kuzingatia masharti nafuu. Mikopo hiyo itatumika kwenye miradi ya maendeleo yenye kuchochea ukuaji wa uchumi.

3.1.9           Mchango wa Mwajiri (Serikali) kwenye Mifuko ya Hifadhi ya  Jamii

64.        Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuwasilisha kwa wakati michango ya kisheria ya mwajiri ya kila mwezi kwa ajili ya watumishi wa umma kwenye Mfuko Mpya wa Hifadhi ya Jamii utakaochukua nafasi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iliyounganishwa ya PSPF, GEPF, LAPF na PPF pamoja na mifuko ambayo haitaunganishwa ya NSSF, ZSSF, WCF na Bima ya Afya (NHIF).

65.        Mheshimiwa Spika, ninatumia fursa hii  kuwasisitiza maafisa utumishi wote wanaohusika na kuingiza taarifa za watumishi wa umma kwenye mfumo wa kompyuta wa kutunza taarifa za watumishi wa umma waingize taarifa za watumishi kwa ukamilifu na usahihi ili uwasilishaji wa michango ya mwanachama na mwajiri kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iwe kamili na sahihi kwa kipindi chote cha utumishi na hatimaye kurahisisha malipo ya mafao, pensheni na mirathi wakati wa hitimisho la utumishi wa umma ili kuwaondolea usumbufu watumishi wa umma walioitumikia nchi yao kwa weledi na uaminifu.

3.1.10        Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa za Kifedha

66.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepangakusimamia na kuboresha uendeshaji na utumiaji wa mfumo wa  taarifa za mishahara ya watumishi wa umma (Government Salaries Payment Platform - GSPP) kwa kuunganisha mfumo huo na taasisi za kibenki na mfumo wa pensheni kwa ajili ya urahisishaji wa huduma za mikopo na pensheni.  Aidha, Wizara itaendelea kuunganisha taasisi 260 katika mfumo wa kukusanya mapato yasiyo ya kodi (Government Electronic Payment Gateway System - GePG), ili kuweza kufanikisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali. Vile vile, Wizara itaunganisha mifumo 10 ya kielektroniki ya taarifa za kifedha kwa lengo la kuiwezesha mifumo iweze kubadilishana taarifa.



3.1.11        Usimamizi wa Mali za Serikali

67.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepanga kufanya kaguzi za mali za Serikali katika balozi kumi (10), kufanya kaguzi maalum na kutoa elimu ya utumiaji na utunzaji bora wa mali katika taasisi mbalimbali za Serikali ili kuepusha hasara zinazoweza kuzuilika.

3.1.12        Ununuzi wa Umma

68.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepanga kufanya yafuatayo: kukamilisha uandaaji na kuzindua Sera ya Ununuzi wa Umma pamoja kuanza utekelezaji wa sera hiyo; kukusanya maoni ya wadau kuhusu changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa sheria na kanuni za ununuzi wa umma kwa lengo ya kuzifanyia marekebisho pale itakapohitajika; kuwajengea uwezo maafisa ununuzi na ugavi serikalini juu ya matumizi ya mwongozo wa utekelezaji wa shughuli za ununuzi na ugavi; kuendesha mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi kuhusu  matumizi ya mfumo wa malipo wa EPICOR katika ununuzi; kuandaa mpango kazi wa usimamizi wa ununuzi wa umma katika Serikali Kuu na Mamlaka ya Serikali za Mitaa; na kutekeleza mapendekezo ya taarifa ya tathmini ya ufanisi wa mfumo wa ununuzi wa umma.

69.        Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizopangwa kufanyika ziko katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 98 hadi ukurasa wa 101.

3.1.13        Ukaguzi wa Hesabu za Serikali

70.        Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2018/19, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imelenga kuimarisha ukaguzi wa mapato na matumizi ya Serikali kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na uwazi kwenye matumizi ya rasilimali za umma. Ili kufikia malengo hayo, Ofisi imepanga kutekeleza vipaumbele nane (8) kama ifuatavyo:  kufanya ukaguzi wa mafungu ya bajeti za Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na wahisani; kufanya ukaguzi wa sekta ya gesi, mafuta na madini; kufanya maboresho ya mfumo wa ukaguzi kwa kutumia TEHAMA; na kukagua ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi. Aidha, Ofisi imelenga kufanya ukaguzi wa kiufanisi na kaguzi maalum katika maeneo yatakayoainishwa; kuwajengea wakaguzi uwezo wa kufanya ukaguzi katika maeneo mapya ya ukaguzi kwenye sekta ya gesi asilia na mafuta, sekta ya madini, Serikali mtandao na katika uhalifu wa kifedha kwa kutumia mtandao (Financial crimes auditing). Vile vile, ofisi itaendelea na ujenzi wa majengo ya Ofisi za Ukaguzi katika Mikoa ya Rukwa na Mara.


71.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepanga kutekeleza  yafuatayo: kufanya mapitio na kufuatilia kampuni ambazo Serikali ina Hisa chache na hazijawasilisha gawio serikalini; kufanya uchambuzi wa uwekezaji unaofanywa na Mashirika ya Umma katika Kampuni Tanzu na kampuni nyinginezo; kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kufanya urejeshaji wa viwanda vinavyosuasua na kuwapatia wawekezaji mahiri; kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa madeni ya ubinafsishaji wa iliyokuwa Benki ya NBC; kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mifuko ya Jamii, Taasisi za Fedha pamoja na wadau mbalimbali katika suala zima la uwekezaji na ufufuaji wa viwanda, kampuni na mashamba yaliyobinafsishwa.

72.        Mheshimiwa Spika, Mipango mingine katika kusimamia Mashirika ya Umma iko katika hotuba yanguukurasa wa 102 hadi ukurasa wa 103.

3.1.15         Mafao ya Wastaafu na Mirathi

73.        Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuboresha, kutunza na kusimamia huduma za Pensheni kwa wastaafu wanaolipiwa Hazina ikiwa ni pamoja na kuendelea kulipa kwa wakati mafao na pensheni kwa wastaafu wa Serikali, mirathi na malipo ya kiinua mgongo kwa watumishi wa Serikali walio kwenye mikataba. Aidha, wizara itaendelea kuboresha masijala ya pensheni kwa kuendelea kuhifadhi kumbukumbu za wastaafu kielektroniki, ili kurahisisha malipo kufanyika kwa wakati.

74.        Mheshimiwa Spika, naombanisisitize kwa maafisa utumishi wote wanaohusika kuandaa mapema nyaraka za watumishi wanaotarajia kustaafu na kuziwasilisha Hazina zikiwa zimekamilika ili malipo ya mafao, pensheni na mirathi ya wastaafu wa kawaida yafanyike kwa wakati na kuwaondolea adha ya usumbufu watumishi pindi wanapokuwa wamestaafu. Aidha, nahimiza ofisi zote za umma zitunze taarifa za watumishi wa umma kielektroniki kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao.

3.1.16        Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi

75.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Kitengo cha Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu ya Mwaka 2012 na Sheria ya Udhibiti Fedha Haramu na Mali Athirika ya Zanzibar ya Mwaka 2009 kwa kutekeleza yafuatayo: kufanya marekebisho ya Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu (The Anti-Money Laundering Act, 2006) na kanuni zake za mwaka 2012 ili kuendana na mahitaji; kuendelea na utekelezaji wa mikakati ya kitaifa na kimataifa ya udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi; kuendelea kupokea na kuchambua taarifa za miamala shuku zinazohusu utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi na taarifa za usafirishaji wa fedha kutoka na kuingia nchini kupitia mipakani; na kuendelea kuwasilisha taarifa za intelijensia kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria.

3.1.17        Tume ya Pamoja ya Fedha

76.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Tume ya Pamoja na Fedha imepanga kufanya uchambuzi wa Mapato na Matumizi yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano.

3.1.18        Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi

77.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepanga kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni za Ubia ili kuimarisha usimamizi wa mifumo ya usimamiaji wa miradi ya ubia na kupunguza mlolongo wa uidhinishaji wa miradi hiyo; kusimamia uibuaji na utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP); kuandaa miongozo ya kitaalam ya kuainisha na kufanya uchambuzi wa miradi ya PPP; na kutoa mafunzo kuhusu utekelezaji wa miradi ya ubia kwenye Wizara, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma na taasisi binafsi.

78.        Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na mamlaka husika inategemea kukamilisha maandiko ya ujenzi wa reli ya Mchuchuma/ Liganga – Mtwara na reli ya Tanga – Arusha – Musoma kwa kiwango chastandard gauge; ujenzi wa miundombinu ya reli katika jiji la Dar Es Salaam kwa ajili ya treni ya abiria na mradi wa kusambaza gesi asilia nchini. Aidha, Wizara itaendelea na hatua ya kutangaza mradi wa ujenzi wa viwanda vya uzalishaji wa madawa muhimu na vifaa tiba chini ya MSD ili kuwapata wawekezaji.

3.1.19        Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma

79.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara kupitia Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma itaendelea kuziwezesha Wizara, Idara Zinazojitegema, Wakala, Taasisi za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kutekeleza maboresho ya usimamizi wa fedha za umma katika maeneo mbalimbali, hususan:  marekebisho ya sheria za kodi  ili sheria hizi ziendane na Sheria ya Uwekezaji; kuhuisha mikataba ya madini ambayo inapata misamaha ya kodi na mfumo wa kufanya maoteo ya viashiria vya uchumi jumla.

80.         Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ya maboresho ni pamoja na: kuandaa na kukamilisha Sera ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini; kuhuisha mikataba ya makubaliano na Washirika wa Maendeleo ili iendane na Sheria za Kodi za Tanzania; kufanya tathmini ya matokeo ya kiutendaji ya mfumo wa vihatarishi katika Wizara, Taasisi, Wakala na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani; kuanzisha Ofisi mpya za Mhakiki Mali wa Serikali katika mikoa ya Simiyu, Katavi na Songwe; kufanya marekebisho ya sheria ya Udalali ya mwaka 1928; nakuimarisha ununuzi wa Umma.


3.1.20        Mradi wa Kimkakati wa kuongeza mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa (Strategic Revenue Generation in LGAs Project)

81.        Mheshimiwa Spika, kupitia Mradi huu, Wizara itatoa fedha katika Serikali za Mitaa zitakazokidhi vigezo vya miradi ya kimkakati ya kuongeza mapato ya Serikali za Mitaa. Aidha, Wizara imepanga kutoa mafunzo  kwa wawezeshaji wa kitaifa juu ya Usimamiaji na Uandaaji wa Miradi ya Kimkakati ya kuongeza mapato kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

3.2       USIMAMIZI NA URATIBU WA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA CHINI YA WIZARA

82.        Mheshimiwa Spika, mipango na malengo ya bajeti kwa mwaka 2018/19 kwa upande wa mashirika na taasisi za umma zilizochini ya wizara ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 109 hadi ukurasa wa 127.

4.0       MAKADIRIO YA  MAPATO NA MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/19

4.1       MAKADIRIO YA MAPATO

83.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara inakadiria kukusanya maduhuli kiasi chashilingi bilioni 597.81 kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mauzo ya nyaraka za zabuni, kodi za pango,  mauzo ya leseni za udalali, gawio, marejesho ya mikopo na michango kutoka katika Taasisi na Mashirika ya Umma.

4.2       MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/19

84.        Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha na Mipango imepanga kutumia kiasi cha jumla ya shilingi12,058,714,013,500 (Bilioni12,058.71kwa mafungu yote nane.  Kati ya fedha hizo, shilingi10,763,501,474,000 (Bilioni10,763.50 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 1,295,212,539,500 (Bilioni1,295.21ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Matumizi ya Kawaida yanajumuisha shilingi 65,764,075,000 (Bilioni 65.76kwa ajili ya mishahara, shilingi 693,257,399,000  (Bilioni 693.26)kwa ajili ya matumizi Mengineyo (OC) na shilingi 10,004,480,000,000(Bilioni 10,004.48ni malipo ya deni la Serikali na michango ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Aidha, katika fedha za matumizi ya maendeleo, shilingi1,266,033,128,500 (Bilioni1,266.03ni fedha za ndani nashilingi 29,179,411,000 (Bilioni29.18ni fedha za nje.

MAOMBI YA FEDHA

4.2.1           FUNGU 50 – WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO

85.        Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:

(a)        Matumizi ya kawaida - Shilingi57,022,927,000 (bilioni 57.02).Kati ya hizo:
(i)          Mishahara - Shilingi 7,577,332,000 (bilioni 7.58)
(ii)         Matumizi mengineyo –Shilingi   49,445,595,000(bilioni 49.44)

(b)       Miradi ya Maendeleo - Shilingi28,790,817,000  (bilioni 28.79). Kati ya hizo:
(i)          Fedha za Ndani - Shilingi19,642,535,000           (bilioni 19.64).
(ii)         Fedha za Nje - Shilingi 9,148,282,000 (bilioni 9.15).


4.2.2           FUNGU 21 - HAZINA

86.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:    

(a)       Matumizi ya Kawaida – Shilingi 531,890,056,000 (bilioni 531.89). Kati ya fedha hizo:
(i)          Mishahara ya fungu hili -Shilingi 21,467,017,000 (bilioni 21.47).
(ii)         Matumizi Mengineyo –Shilingi 510,423,039,000.00 (bilioni 510.42) ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya idara, taasisi zilizo chini ya Fungu hili, pamoja na matumizi maalum.

(b)       Miradi ya Maendeleo – Shilingi 1,247,611,267,500        (bilioni 1,247.61). Kati ya hizo:
(i)          Fedha za Ndani - Shilingi 1,236,190,593,500      (bilioni 1,236.19)
(ii)         Fedha za Nje - Shilingi 11,420,674,000 (bilioni 11.42)

4.2.3           FUNGU 22- DENI LA TAIFA

87.        Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a)         Matumizi ya kawaida – Shilingi 10,013,706,140,000    (bilioni 10,013.71). Kati ya fedha hizo:
(i)           Mishahara - Shilingi 9,226,140,000 (bilioni 9.23)
(ii)         Matumizi Mengineyo (Malipo ya Madeni na Michango ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii) –Shilingi 10,004,480,000,000 (bilioni 10,004.48)

4.2.4           FUNGU 23 – MHASIBU MKUU WA SERIKALI

88.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a)        Matumizi ya Kawaida - Shilingi 46,725,409,000                    (bilioni 46.72).          Kati ya fedha hizo:
(i)           Mishahara – Shilingi7,908,675,000 (bilioni 7.91)
(ii)         Matumizi Mengineyo -Shilingi Shilingi 38,816,734,000 (bilioni 38.82)
(b)        Miradi ya Maendeleo – Shilingi 3,200,000,000.00
          (bilioni 3.20).     Kati ya fedha hizo:
          (i)      Fedha za Ndani - Shilingi 2,000,000,000.00                                                 (bilioni 2.00).
          (ii)     Fedha za Nje  - Shilingi 1,200,000,000.00                                           (bilioni 1.20).




4.2.5           FUNGU 7 –          OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

89.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:

(a)        Matumizi ya kawaida – Shilingi54,592,065,000.00             (bilioni 54.59). Kati ya fedhahizo:-
(i)           Mishahara - Shilingi2,362,279,000.00  (bilioni 2.36)
(ii)         Matumizi Mengineyo -Shilingi Shilingi52,229,786,000.00(bilioni 52.23).
(b)        Miradi ya Maendeleo – Shilingi 1,650,000,000.00                 (bilioni 1.65).          Kati ya fedha hizo:
          (i)      Fedha za Ndani – Shilingi 1,000,000,000.00                                                (bilioni 1).
          (ii)     Fedha za Nje  - Shilingi 650,000,000.00 (bilioni 0.65).

4.2.6           FUNGU 10 – TUME YA PAMOJA YA FEDHA

90.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a)                   Matumizi ya Kawaida -Shilingi 2,155,075,000 (bilioni 2.15). Kati ya           fedha hizo:-
(i)          Mishahara - Shilingi 574,933,000 (bilioni 0.57)
(ii)         Matumizi Mengineyo -Shilingi 1,580,142,000             (bilioni 1.58).

4.2.7           FUNGU 13 –        KITENGO CHA KUDHIBITI FEDHA HARAMU

91.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a)             Matumizi ya kawaida - Shilingi 2,015,586,000 (bilioni 2.01).
(b)         Miradi ya Maendeleo – Shilingi 248,363,000 (bilioni 0.25)ambazo ni fedha za nje.

4.2.8           FUNGU 45 – OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI

92.        Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a)     Matumizi ya kawaida – Shilingi55,394,216,000             (bilioni55.39). Kati ya fedha hizo:
(i)       Mishahara - Shilingi16,647,699,000 (bilioni16.65).
(ii)      Matumizi Mengineyo -Shilingi 38,746,517,000(bilioni 38.75).
(b)        Miradi ya Maendeleo – Shilingi13,712,092,000            (bilioni13.71). Kati ya fedha hizo:
          (i)      Fedha za Ndani – Shilingi7,200,000,000                                                     (bilioni7.20).
          (ii)     Fedha za Nje  - Shilingi6,512,092,000 (bilioni 6.51).
                   
5.0        SHUKRANI

93.        Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuzishukuru nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa ambayo kwa namna moja ama nyingine yamesaidia katika utekelezaji wa bajeti ya Wizara. Aidha, napenda kuwashukuru sana Wafanyakazi na wananchi wote ambao wameendelea kulipa kodi kwa hiari na pia kushiriki katika ujenzi wa Taifa letu.

94.        Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara (www.mof.go.tz).

95.        Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: