MAMLAKA ya Mapato imesema imepata dawa ya kumaliza mianya ya rushwa TRA kwa kuanzisha matumizi ya mfumo mpya wa kielektroniki ambapo wafanyabiashara na walipa kodi watakuwa wakilipa moja kwa moja badala ya kukutana uso kwa uso.

Awali, maafisa wa TRA walikuwa wanakutana na walipa kodi dirishani na maofisini, hali ambayo ilichangia ushawishi wa kutoa rushwa hivyo kuharibu taswira ya TRA na kupunguza mapato ya Serikali sambamba na kuchangia ugumu wa kufanya biashara nchini.

Hayo yalisemwa juzi jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, wakati wa mdahalo wa kupokea changamoto za wafanyabishara nchini ulioandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Uondoaji Umasikini (Repoa) pamoja na mabalozi wa nchi za Nordic.

"Katika jitihada za kupunguza mianya ya rushwa, hivi karibuni tunaanzisha vituo maalum vya kusikiliza kero za walipa kodi wetu," alisema Kayombo na kufafanua zaidi:

"Kwa Dar es Salaam kitaanza hivi karibuni ambapo mlipa kodi atapata nafasi ya kueleza changamoto zake, ambazo zinaweza kutatuliwa hapo hapo zitatatuliwa. Na hii itasaidia mlipa kodi kutokutana na na afisa yule yule ambaye alimhudumia na kumkwamisha."

Kayombo alisema kuna andiko TRA ambalo limezingatia baadhi ya malalamiko ya wafanyabiashara, ambapo moja ya malalamiko hayo ni walipa kodi kulazimika kwenda kwenye ofisi za serikali kulipa kodi zao.

Alisema wafanyabiashara hao wangependa kulipa sehemu moja ili wabaki kuendelea na biashara zao kuliko kupoteza muda kwenda kulipa kodi.

"Mfano mzuri juu ya hili tayari umeanza kujionyesha katika tozo za bandarini kwani mtu anapolipa kodi ya bidhaa zake kutoka nje ya nchini, analipa na gharama za bandari hapo hapo na hatolazimika kulipa kodi halafu akalipe tena Mamlaka ya Bandari," alisema.

"Na hii inampunguzia kero mfanyabiashara ya mzigo wake kukaa muda mrefu bandarini na yeye kupoteza muda."

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye, alisema mdahalo huo ulikuwa na lengo la kupitia hali ya mazingira ya biashara kuona kama yanaimarika au kuzidi kudorora.

Alisema walichokiona ni juhudi ambazo Rais John Magufuli amefanya za kusafisha na kuondoa rushwa na kuongeza hali ya uwajibikaji.

Alisema mwaka jana mwanzoni biashara za ndani kwenda nje zilikuwa chini lakini kwa sasa zimepanda.

"Hivi sasa Rais ametutikisa vya kutosha na watu tumeamua kufanya biashara, lakini kuna mambo tunatakiwa kuyaangalia kwani uaminifu kati ya sekta binafsi na sekta ya umma bado ni mdogo," alisema zaidi Simbeye.

"Na sisi tushamwambia Mh. Rais lakini akatupa changamoto akidai tatizo sisi ni 'wapigaji'... tuongee na wadau wetu waache hiyo tabia."

Alisema wanampongeza Rais Magufuli kwa kukomesha rusha lakini chini bado ipo na imeota mizizi.

Alisema bandarini baadhi ya wafanyabiashara wanapitisha bidhaa zao bila kulipa kodi jambo hilo ndio linakatisha tamaa kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: