Monday, 4 June 2018

Lechantre asema inamlazimu kubadili mfumo wa uchezaji Simba


KOCHA wa Simba, Pierre Lechantre, amesema kwa namna timu hiyo ilivyosajili, inamlazimu sasa kubadili mfumo wa uchezaji wa timu hiyo.

Simba imekamilisha usajili wa wachezaji Marcel Boniventura kutoka Majimaji, Adam Salamba kutoka Lipuli pamoja na Mohamed Rashid kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho.

Akizungumza na Nipashe jana mjini hapa kabla ya kuanza mazoezi ya asubuhi, Lechantre, alisema ujio wa wachezaji hao utamlazimu kutafuta mfumo mpya atakaokuwa akiutumia ukienda sambamba na ule wa sasa uliozoeleka.

"Ujio wa wachezaji wapya utafanya sasa tuwe na 'option' (mbadala) mwingine wa uchezaji, lazima kuwe na mabadiliko ya uchezaji," alisema Lechantre.

Katika mazoezi ya jana asubuhi, Lechantre alimpa mazoezi maalum nyota wake mpya, Marcel na huenda akamtumia kwenye mchezo wa leo.

Simba leo itatupa karata yake ya kwanza kwenye michuano ya SportPesa Super Cup itakapoumana na Kariobang Shark majira ya saa 9:00 kwenye Uwanja wa Afrah.

Akizungumzia mchezo huo, Lechantre, alisema pamoja na kuwa michuano hiyo imekuja katika kipindi ambacho wachezaji wametoka kwenye ligi, watahakikisha wanalibeba jina la Simba.

"Ni ngumu kucheza mashindano kama haya kwa sababu tunawapa presha wachezaji ambao wametoka kufanya kazi ngumu kwenye ligi, lakini tupo tayari na tutahakikisha tunaliweka juu jina la klabu yetu," alisema.

Aidha, alisema ingawa baadhi ya nyota wake walitarajiwa kuwasili jana mjini hapa kuungana na wenzao, ameweka wazi hatawatumia kwenye mchezo wa leo.

Nyota waliotegemewa kuwasili jana ni pamoja na winga, Shiza Kichuya, Mzamir Yassin pamoja na Mohamed Rashid.

Kwa upande wake, Kocha wa Kariobang Shark, William Muluya, amesema anaiheshimu Simba kwa kuwa ni mabingwa wa Tanzania na anafahamu wanacheza soka safi.

"Hata hivyo, na sisi tunawachezaji wazuri na tutahakikisha tunapambana ndani ya dakika 90, hatuwezi kusema tutacheza mchezo gani, kikubwa haya ni mashindano ya mtoano hivyo ni kuhakikisha tunapata  ushindi bila kujali aina ya mchezo," alifafanua.

No comments:

Post a Comment