Kocha msaidizi wa mabingwa wa soka nchini Simba, Masoud Djuma, amekanusha taarifa zilizosambaa mitandaoni mapema jana, kuwa amejiuzulu kuifundisha timu hiyo huku akisema yeye bado yupo sana.

Akifanya mahojiano maalum na msemaji wa klabu hiyo Haji Manara mjini Nakuru Kenya ambapo timu hiyo ipo, Masoud amesema hizo habari si za kweli ni uzushi tu wa watu hivyo mashabiki wazipuuze.

''Sijui haya maneno yametoka wapi, mimi bado nina mkataba na Simba, nimetoka nyumbani kuja kuitumikia Simba na kile kidogo Mungu amenipa nitakitoa kusaidia Simba mpaka mkataba wangu uishe, sina mawazo ya kujiuzulu leo wala kesho labda wanifukuze'', amesema.

Kwa upande mwingine mkataba wa kocha mkuu wa Simba Pierre Lechantre unamalizika June 18, lakini bado haijawekwa wazi kama ataongezewa mkataba au ataondoka. Lechantre alisaini mkataba wa miezi sita na klabu hiyo kukiwa na kipengele cha kuongezewa endapo watajiridhisha na kazi yake.

Timu ya Simba kwasasa ipo mjini Nakuru Mkoa wa Bonde la Ufa nchini Kenya kwenye michuano ya SportPesa Super Cup ambayo imefikia hatua ya nusu fainali baada ya kushinda robo fainali kwa penati dhidi ya Kariobangi Sharks.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: