Thursday, 7 June 2018

Kagame na Arsenal kuchunguzwa


Wanasiasa nchini Uholanzi na baadhi ya Wabunge wa Uingereza na Ujerumani, wametaka kufanyika kwa uchunguzi kuhusiana makubaliano ya hivi karibuni yaliyofikiwa na Serikali ya Rwanda kuidhamini klabu ya soka ya Arsenal ya nchini Uingereza.

Uamuzi huo umejitokeza baada ya kuwepo kwa wasiwasi kuhusiana na mkataba huo wa mamilioni wakati mataifa hayo yakitoa msaada mkubwa kwa Rwanda.

Mkataba huo wa udhamini wa miaka mitatu unaojulikana kama Visit Rwanda, unahusu nembo ya Rwanda kuonekana kwenye jezi za timu ya Arsenal ambapo lengo likiwa ni kutangaza vivutio vya utalii vya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Wakosoaji wamehoji kwanini serikali ya Rwanda imetumia Paundi za Kiingereza milioni 30 kusaini makubaliano hayo na kudai ni fedha nyingi ambazo zingesaidia kuboresha miundombinu na masuala mengine ya maendeleo na kuhakikisha Wanyarwanda wanajikwamua kutoka kwenye umasikini.

Hata hivyo serikali ya Rwanda imesisitiza kwamba fedha hizo za udhamini zimetokana na mapato ya sekta ya utalii yenyewe na inaamini uamuzi huo utachangia pakubwa kuinua sekta hiyo.

Utalii ndio sekta inayoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni nchini Rwanda kiasi cha Dola milioni 400 kwa mwaka ambapo nchi hiyo imepanga kuongeza mapato hayo maradufu na kufikia Dola milioni 800 ifikapo mwaka 2024.

No comments:

Post a Comment