Wednesday, 6 June 2018

Ishara za ndege iliotoweka na abiria 10 nchini Kenya zapatikana

Picha ya mtandao

Ishara za simu kutoka kampuni ya ndege ya FlySax ambayo ilitoweka siku ya Jumanne jioni zimepatikana katika eneo la Aberdares katika kaunti ya Nyandarua nchini Kenya.

Naibu mkurugenzi wa shirika la wanyama pori nchini anayesimamia maeneo ya milima Simon Gitau siku ya Jumatano aliambia shirika la habari la Nation kwamba wataendelea usakaji wao wa ndege hiyo katika eneo la Kinangop ambapo ishara hizo zimeonekana.

Baadhi ya maafisa wa utafutaji na uokoaji walikuwa wakitarajiwa kusafirishwa kwa ndege kutoka katika uwanja wa Njambini ili kupelekwa katika eneo la utafutaji mwendo wa saa moja alfajiri.

Ndege hiyo nyepesi ya kubeba abiria aina ya Cesna C208 ilio na nambari ya usajili ya Y-CAC kutoka Kitale Magharibi mwa Kenya , ilipoteza mawasiliano na mnara wa kudhibiti ndege muda wa saa kumi na moja jioni siku ya Jumanne katika eneo la Aberdares, yapata kilomita 60 kabla ya kufika eneo ililokuwa ikielekea.

Ndege hiyo iliokuwa ikielekea katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta , iliondoka Kitale, muda mfupi kabla ya saa kumi jioni ikiwa na abiria wanane na wafanyikazi wawili na ilitarajiwa kuwasili Nairobi saa moja baadaye.

Kulingana na taarifa taarifa iliotolewa na mkuu wa mamlaka ya usafiri wa angani nchini Kenya utafutaji wa ndege hiyo ambao ulikuwa ukiendelea ulisimamishwa kwa muda na utaendelea siku ya Jumatano alfajiri.

Hatua hiyo inatokana na hali mbaya ya hewa ambayo imeathiri uonekano wa anga na shughuli za maafisa wa uokoaji, Ndege hiyo inasimamiwa na kampuni ya ndege ya East Africa Safari Air Express,

Taarifa kutoka kwa kampuni hiyo zinasema kuwa ndege hiyo ilitoweka lakini juhudi za pamoja zinazoshirikisha mashirika ya wanyama pori KWAS na kitengo cha kuchunguza ajali za ndege zimekuwa zikiendelea kuisaka ndege hiyo.

Ndugu na jamaa wa abiria wametakiwa kusubiri katika hoteli ya Weston iliopo jijini Nairobi.

No comments:

Post a Comment