Saturday, 9 June 2018

Barabara za Sabasaba, Kiseke hadi Buswelu kujengwa kwa lami

Halmashauri ya Manispaa  Ilemela imetia saini na Kampuni ya Sinohydro Corporation LTD kwa makubaliano ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye  jumla urefu wa kilomita 12.1 imegharimu zaidi ya shilingi bilioni 18.

Akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiseke Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo John Wanga  amesema kuwa ujenzi huo utaambatana na uwekaji wa taa za barabarani na sehemu ya uwekaji wa birika za taka ngumu.

 "Mradi huu unahusisha ujenzi wa Barabara za Sabasaba, Kiseke hadi Buswelu kilomita 9.7 Isamilo Big bite hadi Mji mwema kilomita 1.2 na  Makongoro Junction Mwaloni mpaka Kigoto kilomita 1.2 ambapo kampuni hiyo imethibitisha kuwa utekelezaji wa mradi utaanza Juni, 15 Mwaka huu na utadumu kwa muda miezi 15 na kisha kukabidhiwa kwa TARURA, alisema Wanga.

Wanga alisema ujenzi wa barabara hizo zitafungua mianya ya kibiashara na zitarahisisha usafiri ambao ni adha kubwa jambo litakalochangia kuinua uchumi katika Wilaya ya Ilemela.

Mratibu wa TARURA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Kokoya Fuko alimshukuru Rais Dk. John Magufuli kwani ahadi yake anaitekeleza  kwa wakati na kuahidi kushirikiana na viongozi ili kuhakikisha zoezi hilo linaenda vizuri.

 Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Renatus Mulunga aliwaomba wananchi kuendelea kuiamini Serikali ya Awamu ya Tano ambapo imejikita kwenye vitendo zaidi ikiwa ni sambamba na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Kwa upande wake Jin Bin Mwakilishi kutoka Kampuni ya Sinohydro Corporation LTD kutoka nchini China, aliwashukuru viongozi na wananchi kwa kuwaamini, huku akitoa ahadi kutekeleza mradi huo kwa wakati na kwa kiwango cha hali ya juu.

Baadhi wananchi waliohuduria hafla hiyo ambao ni Wakazi wa Kata tofauti ambazo zitanufaika na mradi huo, walitoa shukrani kwa viongozi wao huku, Mkazi mmoja aliyetambulika kwa jina la Mama Magdalena  alisema kuja kwa mradi huo ni ni ajira moja wapo kwa vijana na kuwaomba wajiunge wachape kazi kama Kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano isemayo "Hapa Kazi Tu"

No comments:

Post a Comment