Jeshi  la Polisi Mkoa wa Geita, limemuua kwa kumpiga risasi mtu anayedhaniwa kuwa kiongozi wa kundi la watekaji na wauaji wa watu wanaotekwa kwa lengo la kujipatia fedha.

Polisi ilisema jana kuwa mtu huyo aliuawa wakati alipojaribu kuwatoroka punde baada ya kuonyesha mashimo mawili yaliyokuwa na miili ya watu aliowaua baada ya kuwateka.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake mjini Geita, Kamanda wa Polisi Mkoa, Mponjoli Lotson alimtaja marehemu huyo kuwa Panda Kinasa.

Alisema aliuawa juzi wilayani Bukombe mkoani Geita kwa kupigwa risasi baada ya kupewa onyo na kukaidi kusimama.

Kamanda Mpojoli alisema Kinasa alipigwa risasi kwenye tako na alifaraiki dunia wakati akikimbizwa kwenda Hospitali ya Bukombe, kutokana na kupoteza damu nyingi.

Mwezi uliopita katika nyakati tofauti, alisema kamanda huyo, mtuhumiwa alivamia nyumba ya mfugaji Mbuga Siga katika kijiji cha Ikuzi Lunzewe wilayani Mbogwe usiku wa saa tatu na kumteka mchunga ng'ombe wake Renard Samwel mwenye umri wa miaka 18.

Akisimulia zaidi, Kamanda Mponjoli alisema baada ya kutekeleza utekaji huo, mtuhumiwa aliacha karatasi yenye ujumbe na namba ya simu 0752 901908 akielekeza kutumiwa Sh. milioni 2 kwenye namba hiyo ili aweze kumuachia huru mateka.

"Familia ilitoa taarifa polisi na kufunguliwa jalada ambapo upelelezi ulianza kwa kufuatilia namba hiyo kupitia kitengo maalum cha Jeshi la Polisi kinachohusiana na makosa ya uhalifu wa mitandao ili kubaini alipo mtuhumiwa," alisema.

Wakati polisi ikiendelea na upelelezi wa tukio hilo, Mei 7 saa saba za usiku mtuhumiwa alivamia tena katika kitongoji cha Bwendaseko, Kijiji cha Buganzu wilayani Bukombe na kumteka Nkwambi Mwandu (25), alisema kamanda huyo.

Baada ya utekaji huo pia aliacha ujumbe na namba ile ile 0752 901908 ukielekeza atumiwe Sh. milioni 7 ili aweze kumuachia Nkwambi, alisema.

Kamanda Mponjoli alisema familia ya Nkwambi ilimudu kutuma Sh. 500,000 kwa mpesa na kisha kuripoti Polisi.

Kutokana na ripoti ya pili hiyo iliilazimu kuendeshwa operesheni maalum ambapo Mei 31 polisi walifanikiwa kumnasa mtuhumiwa kupitia mtandao na baada ya kuhojiwa alikiri kuhusika na matukio yote mawili, alisema.

"Baada ya kumkamata mtuhumiwa alikiri na kuwapeleka makachero wa polisi katika msitu uliopo Kijiji cha Msasa na kisha kuwaonyesha shimo lenye urefu wa zaidi ya futi 20 ambamo mwili wa Renard Samwel ulikuwa umetupwa na kutelekezwa," alisema Kamanda Mponjoli. Mwili huo umetambuliwa na ndugu zake.

Mtuhumiwa Kinasa anayedaiwa na polisi kuwa na ujuzi na ubobezi katika matumizi na kucheza na mtandao wa simu, alidai alimuua Samwel baada ndugu zake kushindwa kumtumia fedha aliyokuwa ameomba ili aweze kumuachia.

"Baada ya kuonyesha mwili huo mtuhumiwa aliwapeleka tena (polisi) katika shimo jingine katika msitu uliopo katika kitongoji cha Ibogolre wilayani Mbogwe na kuwaonyesha mwili wa marehemu Nkwabi Mwandu uliokuwa umetupwa na kutelekezwa kwenye shimo lenye urefu wa zaidi ya futi 30," alisema kamanda huyo na kwamba "nao umetambuliwa na ndugu zake."

Baada ya kuonyesha miili yote miwili, mtuhumiwa Kinasa alimpinga kikumbo mmoja wa askari aliokuwa nao na kuanza kukimbia kwa lengo la kutoroka, alisema zaidi Kamanda Mponjoli na kwamba hata baada ya kupewa onyo la kusimama, alikaidi na ndipo polisi walipomfyatulia risasi na kumpiga takoni.

Mwili wake umehifadhiwa katika Hosptali ya Wilaya ya Bukombe na polisi inaendelea na upelelezi ili kuwatambua washirika wa mtuhumiwa, alisema.

Credit: Nipashe
Share To:

msumbanews

Post A Comment: