Leo imekuwa ni asubuhi njema kwa abiria wa mabasi yaendayo haraka (Udart), baada ya kupanda usafiri huo bure.

Abiria wa mabasi hayo, wamejikuta wakipanda bure kutokana na kudaiwa kuwepo kwa hitilafu katika mfumo wa tiketi.

Madirisha ya vyumba vinavyotumika kukatia tiketi yalikuwa yamefungwa huku mabasi yakiendelea kubeba abiria kama kawaida.

Abiria wengi walionekana kufurahia kusafiri bure, hata hivyo baadhi ya wanaotumia kadi wamejikuta wakilipia usafiri huo kwa kuwa wanatumia mashine maalum za kugonga.

"Kumbe ni bure, sikujua inaniuma kama nikadai vile,"amesema abiria mmoja baada ya kugonga kadi yake.

Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, ofisa mawasiliano wa Udart, Deus Buganywa amesema atatoa taarifa kwa vyombo vya habari baadaye.

Abiria mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Daudi Joshua amesema kupanda usafiri bure kumemfurahisha kwa kuwa anaona ni fidia ya usumbufu wa kusubiri magari hayo kwa muda mrefu.

"Huduma ya usafiri huu haitabiriki, tumekuwa tukipata usumbufu mkubwa, sasa leo sijui wanatoa ofa kusafisha makosa yao," amesema Joshua, mkazi wa  Luguruni Mbezi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: