Monday, 14 May 2018

Waziri Nchemba atoa agizo kwa jeshi la Polisi kuhusu Vibali vya Mikutano


Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza jeshi la Polisi nchini kuruhusu Taasisi za dini kufanya mikutano yao watakapoomba kibali.

Aidha, amesema ni lazima kuheshimu uhuru wa kuabudu wa kila dini uzingatiwe kwa kuruhusu wanafunzi na wafanyakazi kwenda sehemu zao za kuabudu kama ilivyopangwa.

Akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na Kanisa la Waadventista Wasabato jijini Mwanza, Dkt. Mwigulu alisema kuwa mafundisho yanatotolewa na taasisi za dini yanasaidia kuwa na jamii yenye raia wema.

Alisema kwa kuwa Wizara hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia uhuru wa kuabudu, watahakikisha wanazungumza na mashirika n ahata shule ambazo zinawazuia wanafunzi na wafanyakazi kuhudhuria kwenye ibada siku za jumamosi.

‘’Nimeagiza jeshi la Polisi wawape uhuru wa kuabudu kwa sababu mnatengeneza jamii iliyobora lakini pia tutazungumza na wahusika kwenye taasisi za elimu na ajira ili tutoe maamuzi yatakayotolewa yasilete doa kwani kazi hii inasaidia kunyoosha nchi,’’ alisema Dk Mwigulu.

Naye, Katibu Mkuu wa Kanisa hilo Kanda ya Nyanza Kusini, Steven Swita alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya waumini wa kanisa hilo kuzuiliwa kwenda kuabudu siku ya jumamosi kulingana na imani zao.

‘’Kumekuwa na utaratibu wa kupangwa masomo ya ziada na mitihani siku ya jumamosi pamoja na udahili wa wafanyakazi na wasipohudhuria huadhibiwa kwa viboko kwa wanafunzi wa shule za msingi na wale wa elimu ya juu wanafukuzwa shule,’’ alisema Swita

No comments:

Post a Comment